Baraza la Wazee wa Chadema limemkaribisha Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kuwania urais mwaka 2020 kupitia chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Lakini CUF upande wa Maalim Seif, wamesema kwa sasa na mwanasiasa huyo mkongwe hana nia ya kujiunga na chama kingine na wanaamini kesi yao watashinda na chama chao kitakuwa imara zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuhusu hali ya kisiasa nchini, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema, Hashimu Juma Issa, alisema kutokana na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, wameona kuna kila sababu ya Maalim Seif kuhamia katika chama chao na kwamba tayari wamefanya naye mazungumzo ya awali.
“CUF na Chadema ni kitu kimoja, CUF ikipanguka Zanzibar, Chadema tunachukua nafasi na Maalim atachukua nafasi yake ile ile ya kuchukua fomu ya urais Zanzibar pamoja na wabunge wake wote watachukua fomu kwa tiketi ya Chadema.
“Sisi ndio wazee wa chama, hatuogopi chochote, hatuna siri, ajenda zetu ziko wazi kwamba huu ndio mpango wetu, tunajiamini tunachosema na ndicho kitakachokuwa,” alisema Issa.
KAULI YA CUF
MTANZANIA ilimtafuta Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, upande wa Maalim Seif, Mbarara Maharagande, ambaye alisema Septemba 2, mwaka huu wakati wa kikao cha madiwani na wenyeviti wa mitaa wa Dar es Salaam, Maalim Seif aliweka wazi msimamo wake kuhusu chama.
“Maalim (Seif), alisema hakuna sababu ya kufikiria plan B (mkakati) nje ya CUF na imani yake ni kwamba mashauri yaliyopo mahakamani tutashinda pamoja na kupigania haki ya kupokwa ushindi wa urais Zanzibar.
“Kwa hali hiyo CUF itakuwa imara zaidi. Chadema ni washirika wetu katika Ukawa na tunathamini nia yao ya kushirikiana. Suala la Katibu Mkuu kujiunga Chadema kwa sasa hatujafikiria na hata likifikia, vikao vya chama ndiyo vitaamua.
“Kwa maana hiyo hata baada ya kumalizika kwa mashauri haya, Maalim Seif kama atataka kugombea urais mwaka 2020 basi atagombea kupitia CUF,” alisema Maharagande.
MGOGORO WA CUF
Mgogoro uliopo ndani ya CUF ulianza baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu nafasi yake Agosti 2015 wakati ambao chama chake kilikuwa kikimhitaji kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.
Sababu zilizosababisha Profesa Lipumba kuchukua hatua hiyo ni kutokubaliana na uamuzi wa vyama washirika wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea nafasi ya urais.
Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye kabla ya majibu ya barua yake ya kujiuzulu kukubaliwa au kukataliwa, Agosti mwaka juzi, Profesa Lipumba alitangaza kuirejea nafasi yake na ndipo kulipoanza mgogoro ambao unakitafuna chama hicho hadi sasa.
Profesa Lipumba anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kama mwenyekiti halali wa chama hicho.
Hata hivyo CUF upande wa Maalim Seif ililazimika kuunda Kamati ya Uongozi iliyokuwa ikiongozwa na Julius Mtatiro ambaye hadi anaondoka katika chama hicho hakuwahi kutambuliwa kama kiongozi halali.
Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili umesababisha kufunguliwa mashauri zaidi ya matano Mahakama Kuu, huku kila upande ukisubiri uamuzi wa nani atatambuliwa kama kiongozi halali.
UCHAGUZI WA MARUDIO
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema, Issa, alisema hakuna sababu ya kufanyika uchaguzi wa mara kwa mara kutokana na kujiuzulu kwa viongozi, hasa wabunge na madiwani kwa kuwa gharama zinatokana na kodi za wananchi.
Akizungumzia kuhusu Serikali kuhamia Dodoma, alisema hawapingi lakini hawakubaliani na hatua ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu nao kuhamia huko kwa sababu uchumi mkubwa wa nchi uko Dar es Salaam.
“Serikali nzima ikikimbilia Dodoma wakati TRA na kila kitu kiko hapa Dar es Salaam, uchumi wa nchi uko hapa wote wakienda Dodoma ushuru utaibiwa kirahisi,” alisema.
Alimtaka Rais Magufuli kujenga urafiki na wabunge wa Chadema kwa kuwa wanaonekana kama maadui mbele ya viongozi wa kiserikali wakati wamechaguliwa na wananchi.
Pia alisema hivi sasa matamko mengi yanatolewa na wakuu wa mikoa na wilaya huku mawaziri wakiwa hawaonekani wakifanya kazi.
Na Elizabeth Hombo - Mtanzania Dar es salaam