MABASI YAENDAYO MIKOANI SASA KUANZA SAFARI SAA 11 ALFAJIRI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditye amesema baada ya wiki mbili mabasi yanayoenda mikoa mbalimbali nchini yataanza safari zake saa kumi na moja alfajiri.

Nditiye alitoa kauli hiyo juzi alitembelea kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo (UBT), Dar es Salaam kisha kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wakiwamo wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa).

Alisema hakuna sababu ya kuwazuia wamiliki wa mabasi wanaotaka magari yao yaanze safari saa kumi na moja alfajiri ya kwa sababu maeneo mengi ya nchi yapo salama kwa sasa.

Nditiye alitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) na polisi kujipanga ndani ya wiki moja kuhakikisha magari yanayotoka Dar es Salaam kwenda mikoani na yale yanayotoka Mwanza kwenda mikoa mingine yanayotaka kuondoka saa 11 alfajiri yanafanya hivyo.

“Pia, magari yanayotoka Mbeya, Arusha na Dodoma yaanze safari zake saa 11 alfajiri. Tutaendelea kuongeza mikoa ambayo magari yatakiwa kuondoka saa 11 alfajiri kwa jinsi mtakavyoanza na mikoa hii.

“Ukweli ni kwamba sasa hivi maeneo mengi ya nchi yapo salama na hakuna sababu ya mabasi kuondoka saa 12 asubuhi. Muondoke saa 11 alfajiri, jipangeni na wekeni utaratibu mzuri wa magari kuondoka muda huo,” alisema.

Alisema kumekuwa na usumbufu hasa wa mabasi yanayotakiwa kuondoka saa 12 asubuhi kutokana na ukaguzi kufanyika asubuhi muda ambao yanapaswa kuondoka jambo ambalo si sahihi.

Alisema licha ya polisi kutoa maelekezo kuwa yakaguliwe siku moja kabla ya safari kwa ajili ya usalama wa abiria, lakini wamiliki wamekuwa wakikaidi agizo hilo.

“Natoa wito kwa wamiliki wa kupeleka mabasi yao siku moja kabla kwa ajili ya ukaguzi na kuweka stika na asubuhi yakipakia abiria yaondoke kama muda ambao tutakuwa tumekubaliana.

Katibu mkuu wa Taboa, Enea Mrutu alisema wameyapokea kwa mikono miwili maelekezo ya naibu waziri kwenda kwa Sumatra na Polisi na kusema ni uamuzi mzuri wa Serikali.

“Tutamwandikia barua rasmi ya kumpongeza waziri. Kikubwa tunawaomba wahusika walitekeleze hili kwa sababu lilishasemwa sana huko nyuma lakini halikutekelezwa, sasa tuna imani litatekelezwa.

“Niseme tu, jana (juzi) asingekuja Nditiye, Alhamisi kusingekuwa na huduma ya mabasi, huu ndio ulikuwa msimamo wa wajumbe wa mkutano. Lakini tunashurukuru ujio wake na tumewasilisha malalamiko yetu kwa Serikali,” alisema Mrutu.

Alisema ingawa hawakupata taarifa mapema kama atakwenda kutembelea kituo hicho, wajumbe walipanga kukogoma kwa sababu baadhi ya madai yao hayajashughulikiwa.

Alitaja madai hayo kuwa ni ukaguzi wa magari usiofuata mpangalio, “Ubungo kuna ukaguzi, ukifika Kibaha ukaguzi, sasa kwa huu mwendokasi wa 80 hatuwezi kufika mikoani kwa wakati ndio maana tulipeleka mapendekezo liangaliwe upya,” alisema.

Madai mengine ni vibao vya mwendokasi wa 50 katika maeneo ambayo hakuna nyumba wala makazi na kero ya utokaji Ubungo.
Alimshukuru Nditiye kwa kuwahidi kushughulikia kero hizo.

Na Bakari Kiango, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post