Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule
Watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamemvamia mfanyabiashara anayefahamika kwa jila la Burugu Mahangija (44), mkazi wa kijiji na kata ya Lyabukande Shinyanga Vijijini kisha kumpora mali zenye thamani ya zaidi ya milioni tatu.
Tukio hilo limetokea jana Septemba 6, 2018 majira ya saa 2:30 usiku ambapo majambazi hayo yalimvamia mfanyabiashara huyo wakati akiwa kwenye duka lake la dawa za binadamu akiuza dawa baridi ndipo yakamkaba na kufanikiwa kupora mali zinazokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni tatu.
Kwa mujibu wa diwani wa kata ya Lyabukande Joseph Misri, amesema majambazi hao baada ya kumvamia kwa mfanyabiashara huyo, yalikuta wananchi wengine wakiangalia taarifa ya habari na kuwaamuru walale chini na kuwapiga 'kutembeza kipigo kwao' na kuwataka watoe pesa.
Alisema wakati wakiendelea na kipigo hicho ndipo baadhi ya wananchi walifanikiwa kuchomoka na kuanza kupiga yowe na yowe zilipozidi majambazi hayo yakarusha risasi hewani kisha kukimbia kusikojulikana huku yakiwa tayari yameshapora mali.
Akizungumza na Malunde1 blog, Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule, amesema majambazi hayo mara baada ya kumaliza kutekeleza uhalifu huo yalikimbia kusikojulikana huku wakifanikiwa kumkamata mmoja wao.
“Katika uvamizi huo mfanyabiashara huyo hakuumia sana kwani walimkaba tu na kisha kupora mali kwenye duka lake hilo la madawa baridi na Jeshi linaendelea na uchunguzi ili kuwakamata wahalifu wengine kwa kuwa wanafahamika,”alisema Haule.
Alisema chanzo cha tukio hilo ni unyang’anyi mali kwa kutumia nguvu.
Na Marco Maduhu- Malunde1 blog