Makamau wa Rais Samia Hassan amewataka viongozi wa dini kuepuka kuchanganya dini na siasa na kujiepusha na migogoro ya kiutawala ndani ya kanisa kwa kuwa kazi ya kanisa ni kuhubiri amani kwa waumini.
Wito huo aliutoa leo katika ibada ya uwekwaji wakfu maaskofu watano wa majimbo matano, katika kanisa la Pentekoste Motomoto mjini Kigoma.
Aidha aliwataka maaskofu hao kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali kwa kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao katika kazi njema na kwamba ili kufikia maendeleo ni lazima kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu.
"Kigoma ni mashuhuda wa athari za ukosefu wa amani kwa kuwa mmepokea wakimbizi kutoka nchi jirani, ni vyema kanisa likalinda amani ya nchi yetu, lazima kanisa lijiepushe na migogoro ya kiutawala ndani ya kanisa",aliongeza Samia.
"Kazi kubwa ya kanisa ni kuhubiri amani kwa waumini wake na wananchi kwa ujumla, neno la Mungu katika kitabu cha Waebrania 12:14 linasema,tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote , naomba muendelee kuhubiri amani kwa kuwa serikali haipendi kuona mogogoro ya kidini ndani ya mashehebu, baina ya dhehebu na dini nyingine", alisema Makamu wa Rais.
Hata hivyo alisema serikali inalitegemea kanisa kujenga maadili ya jamii kwani vijana wengi wameiga tamaduni za kigeni na kanisa liendelee kupiga vita tamaduni mbaya za nje ili kuwa na kizazi chenye maadili mema.
Katika hatua nyingine aliwapongeza viongozi wa Kanisa hilo kwa kulinda misitu na kuwaomba viongozi wengine kuendelea kutunza mazingira kwa kuwa maeneo mengi yameharibiwa kutokana na watu kukata miti na wote watakaofanya hivyo watasaidia mazingira kuhifadhiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa kigoma Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga alitumia mkutano huo kutoa wito kwa wanaume kutumia fursa ya kwenda kupima afya na kujua afya kwa ajili ya kujua afya na kuanza kula chakula chenye lishe ili kuweza kuwa na nguvu na kuweza kufanya kazi.
Alisema mkoa wa Kigoma una chakula cha kutosha lakini ni moja kati ya mikoa yenye watu wenye utapiamlo pamoja na chakula kilichopo na kuwaomba wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusiana na mlo unaojenga afya.
Kwa upande wake, Askofu mkuu wa Kanisa la Pentekoste Motomoto Ezra Mtanya aliipongeza serikali kwa kazi nzuri ya kuwaletea maendeleo wananchi pamoja na kuzuia wizi wa maliasili, madini na kuwaibia wananchi uchumi wao, ambapo mambo hayo yasingesimamiwa kwa umakini wananchi wangeweza kuhujumiwa na kukosa haki yao.
Pia aliahidi kuwahimiza ananchi na waumini kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sera zilizopo, kwa kufanya kazi pamoja na kuanzisha viwanda kwa mustakabali wa kuinua uchumi na Maendeleo kwa wananchi.
Alisema kwa upande wa kanisa linatekeleza sera ya uanzishwaji wa viwanda kwa kuweka mpango wa kufuga nyuki, kwa kuwa mpaka sasa wanamiliki misitu katika wilaya ya Nzega na Uvinza ili kuanza uzalishaji na wameiomba serikali kuwasaidia kuwawezesha kiuchumi waweze kukamilisha mipango yao.
Aliwataka Maaskofu waliowekwa wakfu leo kuongozwa na roho wa Mungu,na kuyatenda yale yote ambayo hayajafanyika ili kuhakikisha kanisa linakuwa jema kwani wamekabidhiwa nafasi ya ukuhani wa Mungu na wanatakiwa kusimamia haki na kuwafundisha waumini neno la Mungu lililo la kweli na kuwa na umoja na ushirikiano.
Kwa niaba ya serikali Makamu wa Rais amewapongeza maaskofu waliowekwa wakfu na kuwa maaskofu ambao Askofu Bwami Mathias askofu mkuu msaidizi, Askafu Eliasaph Mathayo Eliasaph Mathayo askofu jimbo la Mashariki, Askofu Simon Bikatagu jimbo la Magharibi , Askofu Jackson Maneno Jimbo la Kusini, Askofu Shemu Mwenda jimbo la Kati kwa kuchaguliwa kuongoza majimbo na kuitikia wito.
Makamu wa Rais Mama Samia Hassani ameanza ziara yake mkoani Kigoma jana tarehe 08 Septemba na anatarajiwa kufanya ziara ya siku nne ambapo anatarajia kumaliza ziara yake tarehe 11 Septemba 2018 kwa kuzungumza na Wananchi wa Buhigwe.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma.