Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na amani.
Makonda amesema hayo leo Septemba 15, 2018 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa Jimbo la Ukonga.
"Watu walioteuliwa na tume yetu ya uchaguzi ndiyo wenye haki na mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi na si vinginevyo, tuwasikilize na tukubali matokeo, hakuna mwananchi atakayevumiliwa kwa kufanya vurugu ya aina yoyote ile kwa kisingizio cha kupinga matokeo au kulinda kura,"amesema Makonda.
Kauli ya Makonda imekuja siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi Jimbo la Ukonga unaofanyika kesho.
Amesema wananchi wakapige kura kisha warudi majumbani mwao na kusubiri matokeo.
"Tumejifunza siku za nyuma matatizo na vurugu zinazojitokeza wakati wa uchaguzi,"amesema na kuongeza:
"Hivyo Jumapili watu wajipange wakapige kura kisha waende ibadani au wakasali kisha wakapige kura, baada ya hapo kila mmoja arudi nyumbani akasubiri ushindi wa mgombea aliyemchagua,"amesema Makonda.
Makonda amewataka wananchi wakumbuke asiyekubali kushindwa si mshindani, hivyo wawe tayari kupokea matokeo na kuyakubali.
Na Kalunde Jamal, Mwananchi