Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGODI WA BULYANHULU WATILIANA SAINI MAKUBALIANO NA HALMASHAURI YA NYANG'HWALE KUCHANGIA VIFAA VYA UJENZI VYA MIL 500

Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, umetiliana saini Makubaliano na Halmashauri Wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita kuchangia vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya kusaidia umaliziaji wa ujenzi wa zahanati 32 za vijiji wilayani humo.

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nyang’hwale na kushuhudiwa na Uongozi wa Mkoa wa Geita ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Luhumbi, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Hamim Gwiyama na waandishi wa habari.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Luhumbi amepongeza Mgodi wa Bulyanhulu kwa kuchangia vifaa vya ujenzi kwa ajili ya zahanati hizo huku akimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri Nyang’hwale ahakikishe majengo hayo yanakamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.

 “Hii inamaanisha katika kipindi cha miezi minne tunaweza tukajikuta tunatimiza malengo yetu ya kuwa na zahanati katika kila kijiji katika wilaya ya Nyangh’wale, kwa hiyo nipongeze Mgodi wa Acacia, nawashukuru sana huo ni uzalendo wameweza kuonyesha kwamba haya yanaweza kufanyika, wito wangu kwa uongozi wa wilaya, vifaa vitakuja kuwe na utaratibu mzuri wa ufuatiliaji, inawezekana tukienda vizuri wilaya ya kwanza kumaliza zahanati kila kijiji ikawa ni Nyang’hwale.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Geita amepongeza pia kazi nzuri iliyofanywa na viongozi wa vijiji na wananchi kujenga maboma ya zahanati hizo za vijiji na kuonya viongozi wa vijiji vichache ambavyo bado havikamilisha ujenzi wa maboma ya zahanati.

“Napenda niwapongeze pia viongozi wa vijiji ambao wameweza kuwahamasisha wananchi kuchangia nguvu zao kuchangia mawe, mchanga, kuchimba msingi na kuweka jitihada za kusimamia miradi hii, kwa hiyo wito wangu kwa mkurugenzi kama kuna vijiji watendaji hawafanyi kazi wang’oe mara moja tunataka viongozi wanaoleta matokeo.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyang’hwale Mariam Chaurembo ameahidi kufuatilia kwa karibu mradi wa ujenzi wa zahanati hizo ili zikamilike kwa wakati na kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya hasa za mama na mtoto na kutimiza lengo la serikali kusogezea wananchi huduma muhimu za afya kwenye vijiji vyao.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Japhet Simeo amebainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale ina vijiji 62, na katika vijiji hivyo kuna zahanati 14 na vituo viwili vya afya vya umma. 

“Kwa idadi hiyo tunasema ni asilimia 25 ya wananchi wenye uhakika wa kupatiwa huduma za msingi za afya ndani ya vijiji vyao, na wengine asilimia 75 hulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya hali ambayo inahatarisha maisha hasa ya mama na mtoto kwa maradhi ambayo ni rahisi kuzuiliwa na kutibika huduma inapotolewa mapema.”

Naye Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Benedict Busunzu amesema, “Leo tunafurahi kutiliana saini ya kuchangia vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 500 itakayochangia ukamilishaji majengo ya zahanati kwenye vijiji 32 vya Wilaya ya Nyang'hwale.

 Kama wadau wa Maendeleo mchango wetu unaenda sambamba na malengo ya serikali katika sekta ya afya na kampeni ya kijiji kimoja zahanati moja jitihada zinazolenga kupunguza umbali mrefu wa kufuata huduma muhimu za afya.

Busunzu aliongeza kwamba mapema mwaka huu uongozi wa Wilaya ya Nyang'hwale uliutaarifu mgodi kuhusu jitihada inayozifanya ili kuboresha huduma za afya wilayani humo,

“Uongozi wa wilaya ulisema katika jitihada hizo rasilimali za ziada zinahitajika kutoka kwa wadau ili kukamilisha kampeni ya jitihada hizo za "kijiji kimoja, zahanati moja" ambazo inalenga kuhakikisha kuwa wananchi wote wilayani humo wanafikishiwa huduma za afya kwa urahisi.”

Katika mpango wa serikali wa miaka mitano wa Maendeleo juhudi zinaendelea kuongezwa kuboresha upatikanaji huduma za kuzuia na kutoa matibabu kwa wakati. mkakati wa uwajibikaji wa kampuni ya Acacia kwenye jamii unalenga kuchangia katika maendeleo ya jamii endelevu ambazo zina miundombinu muhimu ya kijamii kama huduma za afya, maji, na usafi wa mazingira.

"Mchango huu ambao Mgodi wa Bulyanhulu unatoa kwa ajili ya kampeni “kijiji kimoja zahanati moja” katika Wilaya ya Nyang'hwale Mkoani Geita, unatanguliwa na michango mingine ambayo tumeshaitoa kama vile fedha kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya afya Mkoani Shinyanga ambako mgodi umetoa dola milioni Moja za Marekani sawa na shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kijiji cha Bugarama na zahanati katika kijiji cha Kakola, katika wilaya ya Msalala. 

Tunatumaini kwamba baada ya kukamilisha, kituo cha Bugarama ambacho ujenzi wake unaendelea kitakuwa na hadhi ya kuwa hospitali ya wilaya na kutoa huduma muhimu ya matibabu ya akina mama na watoto kwenye jamii ya watu zaidi ya 150,000.” Alifafanua Busunzu.
Waliokaa kutoka Kushoto: Meneja Mahusiano Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Zumbi Musiba, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyanghwale Bi Mariam Chaurembo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyanghwale Aloyce Mussa Lumambi, Waliosimama kutoka kulia Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyanghwale Tiberus George Rweyemamu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Fabian Yinza, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Luhumbi, Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale Hamim Gwiyama, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Japhet Simeo, wakiwa katika ukumbi wa mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale wakati wa zoezi la kusaini hati za makubaliano ya mchango mgodi wa Bulyanhulu wa kumalizia ujenzi wa zahanati za vijiji 32 vya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale.
Kutoka Kushoto: Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyanghwale Bi Mariam Chaurembo katika ukumbi wa mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale Mkoani Geita baada ya kusaini na kubadilishana hati za makubaliano ya mchango wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati za vijiji 32 vya Halmashauri ya Nyanghwale, Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyanghwale Aloyce Mussa Lumambi, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Luhumbi, Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale Hamim Gwiyama, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Japhet Simeo.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi Benedict Busunzu akizungumza wakati wa zoezi la utiaji saini makubaliano
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Mariam Chaurembo 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyanghwale Bi Mariam Chaurembo akizungumza
Kutoka kushoto Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale Hamim Gwiyama, akibadilishana mawazo na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Bwana Benedict Busunzu.
Kutoka kulia Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyanghwale Tiberus George Rweyemamu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Japhet Simeo na Msaidizi wa Katibu Tawala Utawala na Rasilimali Watu Mkoa wa Geita Herman Matemu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi akiwa Nyanghwale kwenye hafla ya utiaji wa saini
Picha ya Pamoja kutoka kushoto: Katibu Tawala wa Halmashauri ya Nyang'hwale Fabian Yinza, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyanghwale Bi Mariam Chaurembo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyang'hwale Aloyce Mussa Lumambi, Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale Hamim Gwiyama, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria Mkoa wa Geita Sarah Mwangole, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu, Katibu Tawala Msaidizi Serikali za Mitaa Mkoa wa Geita Sania Mwangakala, Katibu Tawala Mkoa wa Geita Dennis Bandisa, Msaidizi wa Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Mkoa wa Geita Herman Matemu, Meneja Mahusiano Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Zumbi Musiba, na Afisa Mahusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu William Bundala nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale mara baada ya kumalizika kwa zoezi la kusaini hati za makubaliano ya mchango wa kumalizia ujenzi wa zahanati za vijiji 32 vya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale

Kushoto: Mganga Mkuu Mkoa wa Geita Japhet Simeo akisalimiana na Meneja Mahusiano Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Zumbi Musiba

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com