Mazishi ya aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Misanya Bingi yamefanyika leo Jumatano Septemba 19, 2018 katika makaburi ya ukoo katika mtaa wa Miyuji jijini Dodoma na kuhudhuriwa na mamia ya watu.
Akiongoza ibada ya mazishi Paroko wa Parokia ya Mpamaa wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dodoma, Valensi Mashuhuli amesema binadamu kuwa msomi au kutokuwa na elimu lakini kama hatajali wengine, bado maisha yake hayatakuwa na maana mbele ya Mungu.
Amesema jambo jema ni kutenda mazuri ya kumpendeza Mungu na kuishi kwa kuombeana wakati wote huku kila mmoja akimchukulia wenzake kama watu wanaotegemeana.
"Huyu ndugu alikuwa ni msomi kama tulivyosikia, lakini katika Mungu tunafurahi maisha yake akiwa hai kwamba alikuwa kielelezo cha utu wema na ndiyo maana tumekusanyika hapa, tafadhari tukaishi hivyo na kujitoa zaidi kwa kila hali mbele za Mungu," amesema Mashuhuli.
Msemaji wa familia, Emanuel Nyanje amesema kifo cha msomi huyo ni pigo kwa kuwa baba wa marehemu, Dismas kabla ya kifo chake aliwaita ndugu na kumteua Dk Bingi kuwa kiongozi wa familia licha ya kuwa alikuwa na umri mdogo.
Social Plugin