Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFIA MIKONONI MWA POLISI...WENYEWE WADAI ALIFANYA JARIBIO LA KUJIUA AKIWA MAHABUSU


 Sakata la watuhumiwa kufia mikononi mwa polisi sasa limehamia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola baada ya familia moja mjini Moshi kukataa kuchukua maiti ya ndugu yao ambaye wanadai alifia mikononi mwa walinzi hao wa usalama.

Waziri huyo amekuwa akikumbana na maswali bungeni na kwenye mikutano na waandishi wa habari kuhusu ongezeko la matukio ya watuhumiwa kufia mikononi au vituo vya polisi na hivi karibuni alijibu kuwa si kila anayefia polisi hutokana na makosa ya polisi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi linadai mtuhumiwa huyo, Andrew Kiwia (pichani) ambaye ni dereva wa Toyota Hiace na mkazi wa Mnazi Moshi, alifariki katika jaribio la kujinyonga akiwa mahabusu ya kituo kikuu cha wilaya, maelezo ambayo familia hiyo haikubaliani nayo kwa madai kuwa maiti ina jeraha kichwani.

Wakati Polisi wakidai alifanya jaribio la kujinyonga akiwa mahabusu na walipomchukua ili kumpleka hospitali kuokoa maisha yake alifariki njiani, ndugu wanadai alifariki kutokana na kipigo cha askari.

Taarifa zinadai Andrew alikamatwa na polisi waliokuwa doria saa 5:00 asubuhi Ijumaa iliyopita akiwa mwenzake, Obasanjo Kitwi, jirani na stendi ya Kiborloni na kupelekwa kituo cha kikuu.

Vyanzo kutoka ndani ya polisi vinadai kuwa mtuhumiwa huyo na mwenzake walikamatwa wakiwa na pombe aina ya gongo, lakini ndugu wamepinga taarifa hiyo wakidai alikamatwa wakati akimnyoa nywele Obasanjo na taarifa za kifo hicho zilijulikana Jumatatu saa 3:30 asubuhi.

Hata hivyo, bado haijafahamika mtuhumiwa huyo aliwezaje kujinyonga kwa kutumia suruali yake aina ya jeans akiwa mahabusu, bila wenzake kushuhudia na kutoa taarifa kwa polisi wa zamu.

“Natamani kuonana na Waziri Lugola kuhusu suala hili,” alisema Haika Mesia Kimambo ambaye ni mama wa marehemu, alipozungumza na Mwananchi nyumbani kwake eneo la Mnazi jana.

Haika alihoji iweje mwanaye achukuliwe na polisi akiwa hai na kisha wakabidhiwe akiwa amekufa na kuhoji kama polisi pamegeuka mahali pasipo salama kwa maisha ya raia.

“Mtoto wangu hajawahi kukutwa na kesi yoyote tangu azaliwe. Naomba nikutane na huyo waziri ana kwa ana anieleze kwa nini mtoto wangu anauawa wakati hajafanya tukio lolote la kihalifu.”

Mama huyo alidai kuwa wao kama familia, hawatazika mwili wa kijana wao hadi polisi watakapoeleza kwa nini walimuua mtoto wao kinyama badala ya kumfikisha mahakamani kama alikuwa na kosa.

Taarifa za msamaria mwema

Siku hiyo, raia ambaye hakujitambulisha na ambaye alidai alikuwa kituoni, aliipigia simu Mwananchi kueleza kuwa kuna kuna mtu amekufa akiwa mahabusu kutokana na kipigo.

Mtoa taarifa huyo alidai kulikuwa na jitihada za polisi kutoa mwili wa marehemu ili ndugu ambao walikuwa kituoni hapo tangu asubuhi kufuatilia suala hilo wasiweze kujua.

Via Mwananchi

    Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

    Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com