Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule (katikati) akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa wachimbaji madini katika mgodi wa dhahabu wa Mwabomba
***
Mchimbaji mdogo wa madini aliyefahamika kwa Jina la Sungwa Chalamila (30-40) mkazi wa Nywarwerwe Bulungwa amefariki dunia baada ya kuporomokewa na kifusi cha udongo na Matimber (Magogo) katika mgodi wa wachimbaji wadogo wa dhahabu Mwabomba kijiji cha Mwabomba kata ya Idahina tarafa ya Dakama Halmashauri ya Ushetu wilaya Kahama mkoa wa Shinyanga.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule aliyefika eneo la tukio amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Septemba 11,2018 majira ya saa saba na nusu katika duara namba moja kwenye mgodi wa Mwabomba.
Amesema Sungwa Chalamila alifariki dunia baada ya kuporomokewa na kifusi cha udongo na magogo akiwa chini mita 100 katika shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu huku wenzake watatu wakijeruhiwa.
Kamanda Haule amewataja watu ambao wamepata majeraha mbalimbali mwilini katika tukio hilo kuwa ni Sagoda Yuda,Richard Elias na Mlekwa Sai ambao wameokolewa kwa kushirikiana na jeshi la polisi, wachimbaji wadogo wa eneo hilo na jeshi la Zima Moto na Uokoaji la Halmashauri ya Mji wa Kahama.
"Majeruhi wamekimbizwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama kwa ajili ya matibabu na hali zao zinaendelea vizuri",alieleza Kamanda Haule.
"Majeruhi wamekimbizwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama kwa ajili ya matibabu na hali zao zinaendelea vizuri",alieleza Kamanda Haule.
Ameongeza kuwa tukio hilo limetokea katika duara namba moja linalomilikiwa na wanachama wanne ambao ni Sengerema Yahururuka,David Jaba Masai Said na Masoud Ramadhan.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog