Mjukuu wa Malkia wa Uingereza, Prince William ametua nchini Tanzania jioni ya leo Septemba 26, 2018 kwa ziara maalum ya siku tatu ambapo kesho Septemba 27, anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es Salaam.
Prince William katika kukutana na Rais Magufuli atafanya mashauriano kuhusu juhudi zinazochukuliwa na Tanzania katika kukabiliana na ujangili na ulanguzi wa wanyama pori.
Prince William ametua mchana wa leo na ujumbe wake ambapo amepokelewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Katiba Sheria Profes Kabudi pamoja na viongozi wengine akiwemo Balozi wa Uingereza hapa Nchini na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini.
Akiwa uwanjani hapo wa Mwalimu Julius Nyerere eneo la wageni mashuhuri, Prince William amepata wasaha wa kuteta na viongozi hao kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa ratiba ya Mwanamfalme huyo, kesho hiyohiyo ya Septemba 27, anatarajiwa kutembelea bandari ya Dar es salaam katika kitengo cha Polisi Marine (Marine Polisi Unit) na ambapo pia atatembelea maeneo mbalimbali ikiwemo yale ya kupokelea mizigo, upekuzi na ukaguzi wa vinavyoingia na kutoka katika eneo hilo la bandari.
Pia Prince William anatarajiwa kukutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla katika ofisi ndogo ya Wizara hiyo Mpingo Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Prince William na ugeni wake huo unatarajiwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na baadae Chuo cha Wanyamapori cha Mwika (College of African Wildlife Management, Mwika (CAWM), kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro na kisha kuendelea na ziara yake nchini Kenya.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa lengo kuu ya ziara hiyo ya Prince William ni pamoja na kufuatilia juhudi za kukabiliana na ujangili na uhifadhi wa wanyama.
Prince William atafanya ziara hiyo katika wadhifa wake kama rais wa mashirika yanayotetea uhifadhi wa wanyama ya United for Wildlife na Tusk Trust.
Amekuwa pia mlezi wa shirika la Royal African Society linalolenga kukuza uhusiano kati ya Afrika na Uingereza na hushiriki sana juhudi za kukabiliana na ujangili.
Na
Andrew Chale, Dar Es Salaam
Mjukuu wa Malkia wa Uingereza, Prince William akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla alipowasili Nchini leo Septemba 26, 2018 kwa ziara maalu. Kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na kushoto Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Sarah Cooke.
Mjukuu wa Malkia wa Uingereza, Prince William akisalimiana na Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki waliomwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Augustino Maige. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla.
Mjukuu wa Malkia wa Uingereza, Prince William akisalimiana na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na kushoto kwake ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla. Wakati Prince William alipowasili Nchini leo Septemba 26, 2018 kwa ziara maalumu.