Waandishi wa habari waliokuwa katika msafara wa ziara ya Rais John Magufuli wilayani Meatu mkoani Simiyu wamepata ajali baada ya gari walilokuwa wamepanda kugongwa na gari jingine leo Jumapili Septemba 9, 2018.
Waandishi waliopelekwa Hospitali ya Wilaya ya Meatu kupatiwa matibabu ni Berensi China na Masunga Samson wa ITV, Aidan Mhando (Channel Ten) na Faustin Fabian wa Mwananchi.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa gari hilo lililowabeba wanahabari liligongwa kwa nyuma na gari jingine wakati likiingia stendi ya mabasi ya Meatu, kwamba wanahabari hao wanalalamika kusikia maumivu sehemu mbalimbali mwilini.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Charles Enock amesema wamepokea watu wanne na wanaendelea kuwapatia matibabu.
“Mpaka sasa tumepokea watu wanne na wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao ni njema. Bado tunaendelea kuwaangalia ila hali si mbaya,” amesema.
Takribani siku tano zilizopita waandishi wa habari wanane walipata ajali ya gari katika msafara wa Rais Magufuli, uongozi mkoa wa Mwanza ukajitwisha gharama za matibabu za waandishi hao.
Chanzo- Mwananchi
Social Plugin