Mtoto Aisha Husseni mwenye umri wa miaka minne amekutwa ameuawa kikatili na kisha mwili wake kuchomwa moto kwenye mfuko wa sandarusi na watu wasiojulikana katika Mtaa wa Sukuma Kata ya Mbugani Manispaa ya Tabora.
Tukio hilo la kusikitisha limebainika jana wakati familia ya mtoto huyo wakimtafuta kwa siku mbili bila mafanikio.
“Huyu mtoto kapotea toka saa nane tukamtafuta tukamkosa, tukatoa taarifa msikitini hadi polisi na ndipo nilipopigiwa simu kuwa mtoto amefariki na ndipo tulipofika” amesema Hussen Maulid Baba wa Mtoto.
Baadhi ya viongozi wa serikali ya Kata wameeleza walivyopata taarifa hiyo pamoja na kulaani kitendo hicho.
“Niliwahoji wakasema kwao kulikuwa na sherehe baada ya sherehe watoto walitakiwa kutoka lakini yeye akapotea katika mazingira ya kutatanisha “ameeleza Abdalah Salum Mwenyekiti Mtaa wa Sukuma.
Salum ameongeza kuwa mtoto huyo amechomwa katika maeneo ya sehemu za siri pamoja na kutelekezwa. Kamanda wa polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi wa Polisi Emmanuel Nley, amethibitisha kupokea taarifa za matukio mbalimbali na kesho atatolea ufafanuzi.
Social Plugin