Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kuanzia kesho Jumanne asubuhi Septemba 25,2018 watu wote waliofiwa na ndugu zao kwenye ajali ya Kivuko cha MV Nyerere katika ziwa Victoria watapewa shilingi milioni moja lakini pia wale walionusurika katika ajali hiyo nao watapokea shilingi milioni moja kila mmoja.
Awali serikali ilitoa utaratibu wa kuwapatia shilingi laki tano wote waliofiwa na sasa serikali imesema watu hao watapatiwa tena shilingi milioni moja
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema fedha za rambirambi zinazochangwa na Watanzania kutokana na ajali ya Kivuko cha MV Nyerere zitawafikia moja kwa moja wafiwa kupitia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.
Akaunti maalumu ya kuchangia rambirambi imepewa jina la ‘Maafa Mv Nyerere’ namba 31110057246 iliyopo katika tawi la NMB Kenyatta jijini Mwanza.
Mpaka sasa idadi ya miili ya watu walioopolewa imefikia 226 baada ya miili miwili ya watoto kupatikana leo Septemba 24,2018
Wataalam wa uokoaji kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na wenzao wa kampuni ya Songoro Marines ya jijini Mwanza wameanza kukinyanyua kivuko cha Mv Nyerere.
Tayari sehemu kubwa ya chini ya kivuko hicho kimeanza kuonekana tofauti na awali.