Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kuhusiana
na ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kikifanya safari
zake kati ya kisiwa cha Bugolora na Ukara katika ziwa Victoria Wilayani Ukerewe mkoani Mwanza ambapo watu 131 wanahofiwa kupoteza maisha. Pia Rais
Dkt. Magufuli ametangaza siku nne za Maombolezo kuanzia leo tarehe 21 Septemba
2018.
Rais John Magufuli amehutubia waandishi muda mfupi uliopita na ameeleza kuwa kufikia sasa imethibitika kwamba miili ya watu 131 imeopolewa na bado kuna hofu kwamba wengine wengi hawajapatikana.
Ameeleza kuwa rasmi kivuko hicho cha MV Nyerere kina uwezo wa kubeba abiria 101, lakini kwa takwimu zilizopo sasa zinazojumuisha miili iliyopatikana pamoja na manusura, ni wazi kwamba chombo hicho kilikuwa kimebeba abiria kupita kiasi.
Rais Magufuli ameagiza bendera ya taifa ipepee nusu mlingoti na kutangaza maombolezo ya kitaifa siku nne kuanzia leo.
. Rais Magufuli amedokeza mambo yaliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo kuwa ni pamoja na nahodha wa kivuko hicho kuwa si mwenyewe ila ‘deiwaka’.
Amesema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba watu 100 au 101 lakini ilibeba watu zaidi, “Taarifa za awali, tulizopata kutoka kwa mashuhuda, Kivuko hicho mpaka sasa hivi (saa 1.14 jioni) maiti 131 na majeruhi 40, tayari imefika 171 na maiti bado wako.”
“Hata aliyekuwa anaendesha hiyo feri, siyo nahodha mwenyewe, yeye hakusafiri na inadaiwa amekamatwa na wote wakamatwe,” amesema huku akisisitiza uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wale wote waliohusika.
Katika hotuba yake ya chini ya dakika kumi, Rais Magufuli amewataka wanasiasa kutokutumia msiba huo kisiasa, “Tuviache vyombo vinavyohusika na uchunguzi, vifanye kazi yake, vifanye uchunguzi vitatoa taarifa.”
“Wale watakaobainika watafikishwa mahakamani na vifo vya Watanzania tusivitumie kisiasa, vyombo vyenye utaalamu vitatoa taarifa yake,” ameongeza:
Social Plugin