Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIOFARIKI KWENYE KIVUKO WAONGEZEKA...MITAMBO YA KUNYANYUA KIVUKO IMEWASILI

 
Idadi ya waliokufa katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Septemba 20, 2018 imefikia watu 228 baada ya mwili mwingine kuopolewa leo Jumatano 26,2018.


Watu 41 walinusurika katika ajali hiyo.

Mwili huo umeopolewa ndani ya kivuko na wazamiaji na wataalam wa uokoaji wanaoendelea na kazi ya kunyanyua na kukigeuza kivuko hicho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mv Nyerere, Isaac Kamwelwe amesema kuna uwezekano wa miili zaidi kuopolewa baada ya kivuko kunyanyuliwa na kugeuzwa.

Tayari Mitambo na vifaa maalum vya kunyanyua, kubeba na kuvuta vitu vizito imewasili katika gati ya Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe tayari kufanya kazi ya kunyanyua na kugeuza kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka katika ziwa Victoria.

Mpaka kufikia jana wataalam wa uokoaji na masuala ya majini walifanikiwa kukilaza ubavu kivuko hicho ambacho awali kililala kifudifudi tangu kilipopinduka Septemba 20.

Mitambo na vifaa hivyo vimewasili asubuhi ya leo vikiwa ndani ya meli mbili kubwa binafsi za Mv Nyakibaria ya kampuni ya Mkombozi and Fisheries na Mv Orion II inayomilikiwa na kampuni ya Kamanga Ferry, zote za jijini Mwanza.

Na Peter Salamba -Mwananchi
CHANZO- MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com