Rais Dk. John Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, kuzitumia fedha za rambirambi zilizobaki zaidi ya Sh milioni 689.99 kati ya Sh milioni 949.6 kujenga majengo matatu ya wodi katika Kituo cha Afya cha Bwisya kilichopo Ukara wilayani Ukerewe, Mwanza.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Kamwelwe wakati akihutubia wananchi, viongozi na wataalamu walioshiriki shughuli ya uokoaji na uopoaji baada ya Kivuko cha MV Nyerere kuzama Alhamisi wiki iliyopita saa nane mchana katika Ziwa Victoria wakati kikitokea Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara kilichopo Ukerewe mkoani Mwanza huku kikidaiwa kubeba idadi kubwa ya abiria na mizigo mingi kuliko uwezo wake.
Pia alisema shughuli ya uokoaji na uopoaji imefungwa rasmi kutokana na kazi ya kukivuta kivuko hicho kukamilika kwa asilimia 100 jana jioni.
Alisema shughuli hiyo imefanikishwa na watu 588 kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika shughuli za uokoaji, uopoaji miili 228 iliyopatikana na watu 41 waliookolewa wakiwa hai hadi inakamilika na kufungwa rasmi.
“Tumeanza jana asubuhi saa 5:21 kuanza kukivuta lakini tukasitisha kutokana na maboya yaliyokuwa yamejazwa upepo ndani ya kivuko na maji yaliyokuwa yamejaa katika ghamla la kivuko na vyumbani hadi saa 10 jioni tulipoanza na kukamilika saa 11: 15 jioni,” alisema.
Pia alisema Magufuli amewapatia motisha watu wote 588 na Sh milioni 240 zitatumika kuwapa posho ya Sh 400,000 kila mmoja na Sh milioni 266 zilitumika kulipa manusura 41 wa ajali hiyo na waliopoteza ndugu na jamaa zao katika ajali hiyo.
Alisema fedha hizo pia zitatumika kujenga uzio katika makaburi na kuwekwa mnara wa kumbukumbu ili kuweka alama ya kumbukumbu ya tukio hilo.
“Gari aina ya canter lenye namba za usajili T 554 DBA liliopolewa na winchi ya gari la Mwauwasa la Mwanza lililokuwa ndani ya Kivuko cha Orion II la Kampuni ya Kamanga Ferry hadi ufukweni kutolewa ndani ya maji,” alisema.
Pia alisema upokeaji wa michango ya ajali hiyo ulihitimishwa jana saa saba mchana na wasiochangia waelekeze maeneo mengine kunako jielekeza kuna matatizo.
Social Plugin