Polisi mkoani Dodoma inamshikilia mwanafunzi wa Chuo cha Mipango kilichopo jijini Dodoma, James Senya (21) kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya uvunjaji na wizi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Gilles Muroto amesema mwanafunzi huyo amekamatwa baada ya kufanyika doria na kugundua kuwa anashirikiana na wahalifu kuvunja na kuiba katika nyumba za watu.
Amesema mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza katika chuo hicho, amekuwa akiwachorea wahalifu ramani ya kuvunja ambapo wahalifu hao hufika na kuvunja na kupora mali zote kwa kushirikiana na mwanafunzi huyo.
“Hii inaonyesha kuwa hata wanafunzi wanajihusisha na uhalifu badala ya kufuata masomo yeye anajihusisha na uhalifu,” amesema Kamanda Muroto.
Mwanafunzi huyo amekamatwa na watu wengine watano anaodaiwa kushirikiana nao katika uhalifu ambao ni Ayubu Hosea (23), Saudi Mosse (23), Semen Njaid (24), Salum Abdallah (16) na Godfrey Mashauri (26) wote wakazi wa Jiji la Dodoma.
Social Plugin