Watu 19 wamefariki dunia nchini Sudan akiwemo Askofu wa kanisa la Anglikana baada ya ndege ndogo ya abiria kuanguka ziwani wakati ikijaribu kutua huku kukiwa na ukungu mzito katikati mwa Sudan Kusini.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 23 kutoka mji mkuu wa Sudan Kusini kuelekea mji wa Yirol jana, kwa mujibu wa afisa wa serikali, Taban Abel Aguek, ni watu wanne pekee ndio wamenusurika katika ajali hiyo miongoni mwao wakiwemo watoto wawili.
Waliopoteza maisha ni pamoja na rubani wa ndege na msaidizi wake na mtumishi wa shirika la Msalaba Mwekundu na Askofu wa kanisa la Anglikana.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu, ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Juba kwenda mji wa Wau kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ilianguka ikiwa na abiria 40 ambapo wote walinusurika lakini wengi wao wakipelekwa hospitali wakiwa na majeraha makubwa.
Social Plugin