Naibu Waziri wa madini Stanslaus Nyongo ameiagiza kampuni ya uchimbaji Dhahabu ya Geita (GGM) kutekeleza agizo la wizara ya Madini kuwalipa fidia wakazi wa Mjini Geita ambao nyumba zao zilipasuka kutokana na mitetemo inayotokana na milipuko inayofanywa na mgodi huo wakati wa kupasua miamba kwenye uchimbaji wa dhahabu.
Nyongo ameyasema hayo wakati akizindua maonyesho ya teknolojia bora ya uchimba wa madini katika uwanja wa kalangalala mjini Geita.
Aliitaka GGM kuheshimu na kutekekeza maagizo hayo na kuwalipa wananchi hao na kusema kuwa kampuni hiyo ihakikishe na kuepuka kusababisha wananchi kuichukia bila sababu ya msingi.
Naibu waziri huyo aliwaomba wachimbaji wadogo wadogo nchini kote kufika katika Maonyesho hayo kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo teknolojia bora na za kisasa za uchimbaji na uchenjuaji wa Dhahabu.
Aidha,Nyongo alisema wachimbaji wadogo nchini wanatapa changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutoelewa sheria na kanuni za madini na kutokuwa na taarifa za kijiolojia ambazo zinasababisha wakose mikopo katika taasisi za kifedha.
Alitumia maonyesho hayo kukemea watu wachache wasio waaminifu wasiofuata sheria na kutorosha madini na kuikosesha serikali mapato na kueleza kuwa serikali haitawavumilia.
Pia alimshukuru mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel kwa ubunifu wa hali ya Juu kuhusu maonyesho hayo na kuwaomba Wakuu wa mikoa na wilaya zote nchini kuiga mfano huo na kutenga siku maalum kwenye maeneo yao ya kuonyesha mazao yanayolimwa huko.
Na Mutta Robert - Geita