Polisi wanadaiwa kumpiga kwa risasi na kumuua, mtu aliyekuwa kwenye gari aina ya canter, baada ya dereva wa gari hilo kukaidi amri ya kusimama.
Katika tukio hilo lililotokea jana mchana, eneo la Kinyanambo C karibu na mji wa Mafinga, shuhuda wa tukio hilo alisema dereva wa gari hilo alikuwa akiendesha zaidi ya spidi 50 katika eneo ambalo magari hayapaswi kwenda mwendo huo.
Hata hivyo jina la marehemu wala la dereva wa gari hilo halikuweza kupatikana mara moja kutokana na polisi kusema bado wanafuatilia.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, ambaye hakutaka kutajwa jina alisema gari hilo lilisimamishwa na polisi, lakini dereva alikaidi amri ya kusimama ndipo askari hao wa usalama barabarani wakaanza kulifukuza.
Gari hilo lilikuwa linatokea barabara ya Iringa kwenda Mafinga.
Inadaiwa kuwa polisi walipokuwa wanalifukuza gari hilo walipiga risasi kwenye kioo cha ubavuni upande aliokaa abiria na inadaiwa ilimjeruhi kichwani na kufariki dunia.
“Risasi ilimpiga kichwani na kutokea upande wa pili wa kichwa, lakini dereva aliendelea kuendesha huku akiwa ameikumbatia maiti, ili isidondoke, huku miguu ya maiti hiyo ikining’inia nje kwa kuwa mlango wa gari ulifunguka katika purukushani ya gari hilo kukimbia,” alisema shuhuda huyo.
Hata hivyo polisi walipofika maeneo ya Kinyanambo C walipiga risasi katika gurudumu la gari hilo na dereva akalazimika kusimama.
Baada ya gari kusimama, polisi hao walimpakia dereva na marehemu kwenye gari lao na kuwapeleka kituo cha Polisi mjini Mafinga.
Shuhuda huyo amesema baada ya kukamatwa na polisi, dereva alikuwa anawalalamikia polisi akisema;
“Kwanini mmemuua ndugu yangu, kwanini mmemuua ndugu yangu.”
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema tayari amepata taarifa hizo ila analifuatilia kwa undani ili apate habari kamili.
“Ni kweli nimepata taarifa hizo, lakini nazifuatilia ili nijue kwa undani kwa sababu tukio lenyewe linaonekana lina utata,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William alisema anawasiliana na wenzake kujua kwa kina kuhusu taarifa hizo na atatoa taarifa kamili.
Chanzo- MWANANCHI