Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akizungumza Bungeni.
Majibu ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuhusu mahabusu wanaofariki dunia wakiwa mikononi mwa polisi, yamezua mjadala ikipingwa vikali na wanasheria na watetezi wa haki za binadamu akiwemo Rais wa chama cha wanasheria (TLS) Fatuma Karume.
Akizungumza na www.eatv.tv Karume amesema kuwa wananchi wanaamini kuwa Polisi ni mahali salama kuliko sehemu yoyote hivyo vinaporipotiwa vifo wananchi wanaondoa imani na Jeshi hilo.
“Waziri hakutakiwa kujitetea vile mbele ya Bunge kwani utetezi wake umekuwa na hoja hafifu haina mashiko, uhai ni zaidi ya zawadi ambayo Mungu ametujaalia kila mmoja anawajibu wa kulinda uhai wa mwenzake hivyo basi inatakiwa arudi kutoa taarifa ya uchunguzi”, amesema Karume.
Ameongeza kuwa “Maneno yake hayana mantiki kwa sababu kulinganisha matukio mawili tofauti. Polisi wanatakiwa kuhakikisha usalama wa watu waliowashikilia kwa mahojiano na kulinda usalama ndilo jukumu lao”.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema kuwa wananchi wanahoji na wanakuwa na chuki na Polisi kutokana na vifo vya ndugu zao vinavyosababishwa na matumizi ya nguvu yanayofanywa na watunza usalama na ndio sababu ya wao kuchukua maamuzi ya kuchoma vituo.
“Waziri alipaswa kukemea badala ya kuhoji kwa nini wananchi hawachukui hatua kwa vifo vinavyotokea mahali pengine ikiwamo kwenye nyumba za wageni kwani kizungumzia nyumba ya wageni ni tofauti kabisa kwa sababu hakuna mtu mwenye jukumu la kulinda usalama wa wateja”, amesema Henga.
Sakata hilo lilianzia bungeni jana Septemba 13 baada ya Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji kuihoji serikali kuhusu mkakati wake wa kukomesha matukio ya mahabusu wanaodaiwa kufariki dunia wakiwa mikononi mwa polisi.
Akijibu swali hilo, Lugola amesema suala la mtu kufa halichagui mahali anapotakiwa kufia kwani kifo ni mtego, na ahadi ya Mungu na mtu anaweza kufariki mahali popote. “Wengine wanaweza kufia kwenye magari, hospitali, bungeni na hata wengine wanakufa kwenye nyumba wakijamiiana.
Hivi karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ya wananchi kususa maiti za ndugu zao au kuvamia vituo vya polisi baada ya ndugu zao kufariki mikononi mwa polisi ambapo matukio hayo yamejitokeza katika mikoa ya Mbeya na jijini Dar es salaam.
Chanzo- EATV