Rais Dkt. John Magufuli amempandisha cheo Kaimu meneja wa Kampuni ya huduma za Meli (MSCL) Erick Hamis kuwa Meneja mkuu kwa kile alichodai kuwa amependezwa na mikakati yake inayoonesha dhahiri nia yake ya kulifufua shirika hilo na kumpa sharti la kutolewa sifa na kuliua tena shirika.
Rais amefanya uamuzi huo wakati akihutubia wananchi na wafanyakazi wa kampuni hiyo jijini Mwanza baada ya kushuhudia makubaliano rasmi ya mkataba wa ujenzi wa Meli mpya Chelezo, na ukarabati wa Meli za MV Victoria na MV Butiama katika ziwa Victoria na kampuni nne kutoka Korea Kusini, mkataba ambao una thamani ya Shilingi bilioni 152.
Rais Magufuli amesema kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikielekea mwisho na alikuwa mbioni kuifuta kama sio jitihada za kiongozi huyo kuonesha nia katika kupambana na rushwa ambayo ndio kikwazo alichokitaja kuua vyanzo vya mapato, hivyo kumuagiza meneja huyo kuhakikisha hakuna kitakachopotea kuanzia leo anapokabidhiwa majukumu rasmi.
"Enzi zile kulikuwa na wizi, wafanyakazi walikuwa wakiiba mafuta. Mapato yalipokuwa yakipatikana yalikuwa yakipelekwa Dar es Salaam na wafanyakazi wanafahamu". Rais Dkt. Magufuli.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji mradi wa ujenzi wa meli hiyo mpya na ukarabati wa meli nyingine za MV Viktoria na Mv Butiama na ujenzi wa Chelezo, Meneja huyo amesema ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 yenye tani 400 utatoa ajira 250.
Social Plugin