Rais Magufuli ameyasema hayo jana, kwenye mkutano wa hadhara aliofanya wilayani Meatu mkoani Simiyu ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo amesisitiza watanzania waendelee kuzaa lakini wachape kazi ili kuwatimizia mahitaji muhimu watoto wao.
''Najua Waziri wa Afya Ummy Mwalimu hapa angependa kuongelea mambo ya uzazi wa mpango lakini mimi mengine huwa sikubaliani nayo sana, utapangiwaje kuzaa'' ? alihoji Rais katika mkutano huo.
Rais Magufuli alisema amezunguka mataifa mengi duniani na amejionea jinsi yanavyotafuta nguvu kazi kutokana na mambo ya uzazi wa mpango hivyo kuwashauri wananchi kusikiliza na kuchuja baadhi ya mambo.
''Kwahiyo katika kushauriwa mengine tukubali na mengine tukatae tutumie msemo wa mzee Jakaya Kikwete (Akili za kuambiwa changanya na za kwako) kuzaa ni muhimu'', amesema.
Aidha alisisitiza kuwa anajua watapinga sana lakini ukweli ndio huo watu wamejazwa mawazo ya ajabu na kwamba huwezi kuwa mwanaume kisha ukubali kufungiwa kizazi.