RAIS MAGUFULI : TUMELALIWA VYA KUTOSHA NGOJA NA SISI TUWALALIE

RAIS John Magufuli amekemea tabia ya baadhi ya kampuni za uchimbaji madini zinazokwepa jukumu la kusaidia shughuli za kijamii katika maeneo wanayochimba madini, ikiwemo kuchangia fedha katika utekelezaji wa miradi ya maji, afya na elimu. Ambapo amesema kampuni hizo zina wajibu wa kurudisha faida wanayopata katika jamii.


Rais Magufuli wakati akizungumza na akizungumza na Wananchi katika kijiji cha Nyamongo wilayani Tarime mkoa wa Mara jana tarehe 7 Septemba, 2018 amesema baadhi ya kampuni za uchimbaji madini zimekuwa zikiilalia serikali na wananchi kwa ujumla, na kwamba safari hii ni zamu yao kulaliwa.


“Lakini bahati nzuri sasa hivi tumepitisha sheria nzuri ya madini, palikuwa na sheria ya hovyo hovyo ndiyo maana nikasema, tumelaliwa vya kutosha ngoja na sisi tuwalalie, wametugeuza vya kutosha ngoja na sisi tuwageuzie, wametuchezea vya kutosha na sisi lazima tuwachezee, hii mali tumepewa na Mungu na Mungu ndiye alitaka hii mali iwe nyamongo kwa hiyo wale walitakiwa kuyafanya nataka kuwambia watayafanya, kwa hiyo huu mradi wa maji kwa vile ulikuwa ni mradi wao, nitamtuma waziri wa maji akazungumze nao.”


Kauli hiyo imetolewa na Rais Magufuli baada ya kupokea taarifa kuhusu kukwama kwa mradi wa maji unaojengwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia wilayani Tarime mkoa wa Mara unaogharimu kiasi cha Sh. Milioni 700.


Rais Magufuli amesema haiwezekani kampuni hiyo ikapata faida kutokana na uchimbaji madini, halafu ikashindwa kutoa sehemu ya faida hiyo kwa ajili ya kusaidia wananchi husika katika kutatua kero ya maji.


“Huu mradi wa milioni 700 ambao walisema wataleta na hawajaleta, mimi mwenyewe nitadili nao, kwa sababu hakuna mwekezaji aliyekuja kutangaza dini huku. Wote wamekuja kuwekeza kwa sababu ya kutafuta faida, sasa hawawezi wakataka faida, hata ile faida kidogo tunayoitaka na yenyewe waichukue, kwa sababu milioni 700 ni kiasi gani kwa mgodi mkubwa unaochukua matrilioni ya fedha? Maji tukose, wao wanakunywa maji ya chupa, hawataki kutupa maji miaka yote wanachukua dhahabu sisi kutupa maji hapana, nasema hili tutalisimamia,” amesema na kuongeza Rais Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post