RC GAGUTI ATAKA VIONGOZI WA NYUMBA KUMI WATUMIKE KWENYE ZOEZI LA UTOAJI VYETI KWA WATOTO


Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia jenarali Marco Gaguti akizungumza wakati wa semina kwa viongozi wa wilaya na mkoa huo, kuhusu mpango wa usajili wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

 ****
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amezitaka halmashauri za wilaya kuweka utaratibu wa kutumia nyumba kumi katika maeneo yenye historia ya kuwa na watu wengi wasio raia wa Tanzania ili kuwabaini wakati wa utekelezaji wa mpango wa kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Agizo hilo lilitolewa na mkuu huyo wa mkoa Septemba 14 mwaka huu katika manispaa ya Bukoba wakati wa semina kwa viongozi wa wilaya na mkoa, kuhusu mpango wa usajili wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano katika mkoa huo, unaotarajiwa kuanza rasmi Oktoba 01 mwaka huu.

Gaguti alisema utaratibu wa kuwatumia viongozi wa nyumba kumi kuwabaini walio raia na wasio raia litarahisisha utekelezaji wa zoezi hilo, kwa kupata taarifa sahihi zinazowahusu wazazi wa watoto watakaosajiliwa na wakala wa usajili, ufilisi na udhamini (RITA).

“Kila mtoto anayezaliwa hapa mkoani anapaswa kusajiliwa bila kujali wazazi wake ni Watanzania au sio Watanzania, lakini wakati wa uandikishaji huu inabidi taarifa kuhusu wazazi wa watoto hao ziwe sahihi, na ndizo zitakazoonyesha kuwa wazazi wao sio Watanzania au ni Watanzania”, alisema Gaguti.

Akiwasilisha mada kuhusu usajili huo kwa viongozi hao, Kaimu meneja usajili wa Rita Patricia Mpuya alisema kupitia mpango huo watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano watasajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa, kupitia vituo vya tiba na ofisi za watendaji kata.

Mpuya alisema  zoezi kama hilo limeshafanyika katika mikoa 11 ya Tanzania Bara, ambayo ni Mwanza, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Geita, Shinyanga, Mtwara, Lindi, Mara na Simiyu, na kuwa watoto milioni 2.7 wa mikoa hiyo wamekwishasajiliwa na kupewa vyeti.

Kwa upande wake Kaimu mtendaji mkuu wa Rita, Emmy Hudson, alisema zoezi la kuwasajili na kuwapatia vyeti papo kwa papo litaanza Oktoba 01 mwaka huu katika mkoa wa Kagera, na kuwa wanatarajia kusajili watoto zaidi ya 400,000.

Hudson alisema kuwa watoto hao watapatiwa vyeti vilivyoandikwa kwa mkono ambavyo ni vya kudumu, na kuwa mtoto anaweza kubadilishiwa cheti kwa kwenda katika ofisi za halmashauri,endapo alichopewa kitapotea au kitapata uharibifu wowote ule.

“Vyeti hivi vinaandikwa kwa mkono, lakini vinatambuliwa kama ilivyo kwa vyeti vingine vilivyochapishwa kwa mashine, baada ya mtoto kusajiliwa taarifa zake zitatumwa katika kanzi data ya Rita, kwa hiyo ni salama”, alisema.

Alisema lengo la kupeleka huduma hiyo karibu na wananchi ni kuhakikisha idadi ya watoto waliona vyeti vya kuzaliwa inaongezeka na kuwa hali ya usajili kwa sasa bado ni duni na ndiyo maana wamekuja na mkakati huo ili kuongeza kasi.

“Wazazi wengi walishindwa kusajili watoto wao kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo umbali wa maeneo ya kusajilia, uelewa mdogo na gharama za ufuatiliaji wa huduma katika ofisi husika, kwa hiyo tunapowafikishia huduma hii katika makazi yao, wataepuka changamoto hizi” ,alisema.

Kwa mujibu wa ofisi ya taifa ya takwimu, idadi ya watoto chini ya umri wa miaka mitano mkoani Kagera kwa mwaka 2018 ni 542,806. Na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 asilimia 12.2 ya watoto mkoani humo ndiyo wenye vyeti vya kuzaliwa, na hivyo watoto wanaopaswa kusajiliwa ni 475,498.

Na Agela Sebastian - Malunde1 blog 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post