Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BAADA YA RC MONGELLA KUSHUTUMIWA KUSITISHA UOKOAJI USIKU..MWENYEWE AELEZA KILICHOTOKEA


Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella ametoa ufafanuzi kuhusu zoezi la uokoaji kusitishwa juzi usiku Septemba 20, 2018 akisema ulitokana na ushauri wa wataalam wa uokoaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 22, 2018 katika mwalo la Kisiwa cha Ukara anakoongoza zoezi la uokoaji, Mongella amesema wazamiaji walishauri uokoaji usitishwe hadi jana asubuhi kutokana hali mbaya iliyoanza kujitokeza chini ya maji nyakati za usiku.

"Zoezi hili linafanyika kitaalam na wazamiaji wabobevu wanaofanya kazi kwa saa 24 ambao ilipofika usiku walishauri watu wasizame tena chini ya maji. Mimi kama msimamizi nisiye na utaalam wa kuzama majini sikuwa na namna nyingine zaidi ya kuwasikiliza," amesema Mongella.

"Nisingetumia kofia yangu ya ukuu wa Mkoa na msimamizi wa zoezi la uokoaji kulazimisha waendelee kuzama kwa sababu uamuzi huo ungeweza kusababisha madhara zaidi ikiwemo kuwapoteza wataalam na kuongeza matatizo zaidi."

Amewasihi Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kuzungumzia kwa busara na staha ajali hiyo kuepuka kuongeza machungu kwa waliopoteza ndugu na kujeruhiwa katika ajali hiyo.

Ufafanuzi huu wa Mongella umekuja katikati ya mjadala miongoni mwa Watanzania kuhusu taarifa za uokoaji kusitishwa usiku wa Septemba 20 kutokana na giza.

Mv Nyerere inayofanya safari kutoka Bugolora kwenda kisiwa cha Ukara kimezama Septemba 20 ambapo hadi sasa maiti zaidi ya 151 zimeopolewa huku watu 40 wakiokolewa wakiwa hai.

Kivuko hicho kina uwezo wa kupakia abiria 101 na tani 25 ya mizigo.

             RC ashutumiwa kusitisha uokoaji

Kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella,  kutangaza kusitisha uokoaji wa watu waliozama kwenye kivuko cha MV. Nyerere katika Ziwa Victoria kwa sababu ya giza, kimeibua mjadala mzito huku wananchi wakihoji sababu za kufanya hivyo.

Juzi saa 8:10 mchana, Kivuko cha MV. Nyerere kilizama kwenye ziwa hilo karibu na bandari ya Ukara kikitokea kisiwa cha Bugorora, wilayani Ukerewe na kusababisha vifo vya watu 126 hadi jana huku wengine 37 wakiokolewa wakiwa hai.

Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu, lakini wakati wa tukio, ilielezwa na mashuhuda kuwa kilikuwa kimebeba pia lori kubwa lililokuwa libeba mahindi.

Wakati shughuli ya ukoaji ikiendelea juzi, ilipofika saa 3:00 usiku, katika hali isiyotarajiwa, Mongella alitangaza kusitisha uokoaji hadi jana asubuhi huku akitaja sababu kuwa ni kutokana na giza.

Baada ya kauli hiyo, kwa nyakati tofauti wananchi wamehoji sababu za kufanya hivyo huku wakivitilia shaka vifaa vya uokoaji vilivyonunuliwa kwenye vikosi vyote vya uokoaji kama vilizingatia uokoaji wa nyakati zote.

"Inasikitisha sana kuona ndugu zetu wamezama ziwani halafu kiongozi mmoja anasitisha uokoaji kisa giza limeingia. Tunapata wasiwasi wa vifaa vya uokoaji vilivyopo ambavyo vimenunuliwa kwa kodi zetu kama wakati wa ununuzi vilizingatia utoaji wa huduma kwa nyakati zote au la," alihoji Mariamu Yusuph kwenye mtandao wa kijamii.

Mariamu aliandika kwenye mtandao wa Facebook kuwa kauli ya Mkuu wa Mkoa inawakatisha tamaa ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa na watu hao ndani ya kivuko hicho.

Naye Rashid Chilumba alielezea kusikitishwa na hatua ya kusitishwa kwa uokoaji kwenye ajali hiyo hadi kesho yake, jambo alilosema kuwa halikutakiwa kufanyika.

Chilumba katika maelezo yake alihoji kuwa: "Sasa kesho mtakwenda kuokoa au kuokota maiti?"

Katika andiko lake, alisema Mwanza kuna kikosi cha jeshi, boti za doria za polisi, helkopta na vivuko vingine na kuhoji kama vyote hivyo havina taa kubwa za kuwezesha uokoaji kuendelea usiku kucha.
Chilumba aliendelea kuhoji kuwa kama vyote havina uwezo huo vilinunuliwa vya kazi gani.

"Ni aibu kwa viongozi kusema tunaenda kulala eti kuna giza ziwani wakati kuna dazeni ya Watanzania wenzetu tunaowahudumia wamezama ziwani tena siyo kwa uzembe wao bali kwa tabia zetu za kutojali maisha ya watu na kusimamia usalama wao," aliandika mtu huyo.

Mchangiaji mwingine kwenye Facebook alihoji kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kamati yake ya ulinzi na usalama walipata wapi ujasiri wa kwenda kulala wakati Watanzania wenzao wako chini ya ziwa.

"Mmepata wapi ujasiri wa kwenda kulala na kuna watu watoto wao, baba zao, mama zao wamo majini na hawajui kama watawapata wakiwa hai, hivi ingekuwa ni jamaa zenu wa karibu mngepata ujasiri wa kusimamisha zoezi kwa sababu ya kiza?" alihoji.

Wasomi nao walielezea kushangazwa na hatua ya kusitisha uokoaji wakati kuna watu ambao bado wako majini, jambo ambalo wamelielezea kuwa halikuwa la kibinadamu kwani walitakiwa kutafuta njia mbadala na siyo kusitisha.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (USDM), Richard Mbunda, alisema serikali ya Mkoa wa Mwanza inastahili kulaumiwa kwa tukio hilo kwani imeshindwa kujipanga katika uokoaji.
Alisema matukio kama hayo yameshawahi kutokea siku za nyuma,hivyo serikali ingetakiwa kuwa na vifaa vya uokoaji pindi ajali inavyotokea katika vyombo vya majini.

"Nilitarajia kuona serikali ingekuwa imejipanga kukabiliana na matukio kama hayo lakini inaonekana uokoaji ulisitishwa juzi usiku kwasababu ya giza. Hizi ni sababu ambazo zinakatisha tamaa wananchi," alisema.

Aliongezea kuwa: "Kuna taarifa ambazo zinasambaa na kuonyesha kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba watu zaidi ya kiwango kinachotakiwa. Hapo  inaonyesha ni uzembe wa hali ya juu hatuna umakini na vyombo vya usafiri baharini."

Mbunda alisema serikali ijipange kuzuia matukio kama hayo matukio ya nyuma yalisababisha hasara kubwa na simanzi kwa wananchi jambo ambalo viongozi walitakiwa kujifunza na kuchukua tahadhari.

Alisema serikali inatakiwa kuweka mkakati endapo likijitokeza tatizo kama hilo ili  kuokoa watu kwa wakati na kuhakikisha vyombo hivyo ambavyo vinamilikiwa na serikali vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Sitole, alisema kitendo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kusitisha uokoaji halikuwa jambo la busara kwani kuna taasisi na vitengo vya uokoaji, hivyo wangetakiwa kuendelea na uokoaji bila kutoa kisingizio cha giza.

"Sidhani kama wangekosa mwanga wa kuendelea kuokoa hao waliozama ina maana kama kulikuwa na watu wanaweza kuokolewa kwa muda huo halafu unasitisha ina maana tunawaacha wafe ndio maana nasema hapakuwa na busara,"alisema

Sitole alisema Mkoa ulitakiwa kufanya jitihada zozote za kuhakikisha wanaendelea na uokoaji usiku kucha badala ya kutoa kisingizio cha giza.

Mkazi wa Mwenge, James Fredy, alisema ingetafutwa njia mbadala ya kusaidia uokoaji badala ya kutangaza kusitisha kwani taarifa hiyo imewaumiza watu wengi ikiwamo wana familia.

"Watu wana matumaini ya ndugu zao kuokolewa halafu serikali inakuja kutangaza kusitisha hivi ingekuwa ni ndugu zao wamezama katika hiyo boti wangesitisha kiukweli hiyo kauli ya kusitisha imetusikitisha sana," alisema.

Alisema kuna haja ya serikali kuwa na vifaa vya uokoaji ili matatizo kama hayo yanapojitokeza wananchi waokolewe kwa wakati.

Aidha, Fredy alisema serikali iwe inachukua tahadhari mapema badala ya kusubiria madhara kutokea Kivuko hicho kilifungwa injini mpya Julai mwaka huu baada ya awali kupata hitilafu na kimekuwa kikitoa huduma zake kutoka Kisiwa cha Bugorora- Ukara wilayani Ukerewe tangu mwaka 2004.

Mei 21, mwaka 1996 meli ya MV. Bukoba ilizama kwenye ziwa hilo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800.
CHANZO - MWANANCHI NA NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com