RPC AAMURU ASKARI KUPIGIA SALUTI WABUNGE...WASIWACHUKULIE WA KAWAIDA


Kamanda wa Polisi mkoani Katavi, Damas Nyanda, ameagiza askari polisi watakaokaidi sheria ya kuwapigia saluti wabunge wa mkoa huo, wachukuliwe hatua. 

Agizo hilo alilitoa jana wakati akizungumza na askari polisi wa mkoa huo wakati wa hafla ya kupokea msaada wa samani za ofisi.

Samani hizo ni meza tatu na viti 17 vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Sebastiani Kapufi, kwa ajili ya Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mpanda.

Alisema ni vizuri askari wa jeshi hilo wakatambua nafasi za wabunge kwa kuwa wapo baadhi ya askari wanapokutana na wabunge hawajali nafasi zao na hawawapigii saluti.

Alisema kuwa Kanuni za Jeshi la Polisi (GPO) namba 102 zinaelekeza viongozi wanaotakiwa kupigiwa saluti wakiwamo na wabunge, lakini baadhi ya askari polisi hawatii sheria hiyo na kusema wasiofanya hivyo wanafanya makosa.

Aliwataka askari polisi kuhakikisha wabunge wote wanao kuwa kwenye majimbo yao, wanapigiwa saluti na hiyo sio hiari bali ni lazima na atakayekaidi atachukuliwa hatua.

"Msiwaone wabunge wenu wa kawaida sana kwa kuwa mmekuwa mkiongea nao, mtambue kuwa wabunge ni viongozi na wanastahili kupewa heshima zao zilizopo kwa mujibu wa sheria," alisema.

Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Kapufi alisema mtu anapokuwa kiongozi hatakiwi kuvunja sheria za nchi kwa kuwa kiongozi ni kioo kwenye jamii.

Chanzo - NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post