Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TIDO MHANDO AMTAJA KIKWETE MAHAKAMANI


Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando amesema Serikali imelipa Sh887.1 milioni kwa watu wasiojulikana tofauti na inavyodaiwa na upande wa mashtaka.

Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.

Amedai alikwenda kufanya kazi TBC baada ya kuitwa na rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na kwamba majukumu yake yalikuwa ni kulibadilisha shirika hilo liwe shirika lenye uwezo na kuheshimika duniani.

Tido ameyaeleza hayo leo Septemba 20, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati akiongozwa na wakili Martine Matunda na Ramadhani Maleta kutoa ushahidi wake wa utetezi katika kesi inayomkabili.

Akitoa utetezi wake mahakamani hapo amedai tuhuma anazotuhumiwa nazo zimemuumiza sana kwa sababu alikuwa na ndoto ya kuifikisha TBC mbali ili iweze kutoa gawio kwa Serikali na si Serikali kutoa fedha kwa TBC.

Kuhusu kuisababishia Serikali hasara ya Sh 887.1 milioni, Tido amedai hakushirikishwa kwa namna yoyote katika malipo hayo na kwamba angeshirikishwa angeweza kunusuru pesa hiyo isilipwe.

Amedai mwaka 2012 aliitwa Takukuru kutoa maelezo na kwamba malipo yanaonyesha kufanyika mwaka 2015 yeye akiwa tayari ni mtuhumiwa na hakuwahi kuitwa popote kuulizwa kuhusu mchakato mzima wa mradi kabla malipo hayo hayajafanyika kwani angeweza kushauri.

Tido aliyeanza kujitetea leo Septemba 20 kuanzia saa tatu asubuhi amemaliza utetezi wake saa sita mchana.
Na Tausi Ally, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com