TUNAHITAJI WAWEKEZAJI KWENYE MAZAO YA KILIMO, SAMAKI NA MIFUGO-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji wawekezaji wakubwa kutoka China ambao watawekeza kwenye viwanda vya mazao ya kilimo, samaki na mifugo.

Aliyasema hayo jana (Jumatatu, Septemba 03 ,2018) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa China, Bw. Han Changfu, jijini Beijing.

Alisema  katika kipindi hiki ambacho Tanzania imeamua kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda, China ni nchi sahihi kushirikiana nayo kwa sababu inawawekezaji wa kutosha.

“China ni rafiki yetu na pia imepiga hatua kubwa kwenye teknolojia ya viwanda, hivyo tunahitaji kuendelea kushirikiana nayo ili tuweze kupata na teknolojia sahihi ya viwanda mbalimbali.”

Waziri Mkuu alisema Serikali zote mbili ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ziko tayari wakati wowote kuwapokea wawekezaji kutoka China.

Alisema wawekezaji hao watapatiwa ardhi ya kujenga  viwanda ambavyo vitatumia mazao ya kilimo, mifugo na bahari hasa samaki  ambayo mengi yanapatikana kwa wingi nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Tanzania inahitaji kupata soko la mbaazi na soya nchini China ili kuwawezesha wakulima wake kuwa na soko la uhakika la mazao hayo.

Alisema Tanzania hivi sasa inakabiliwa  na tatizo la ukosefu wa soko la mazao hayo, baada ya wakulima kuitikia wito wa Serikali  wa kuwataka walime mazao hayo kwa ajili chakula na biashara.

“Tumelazimika kutafuta masoko ya mazao hayo hapa China ili kutowakatisha tamaa wakulima wetu kwani itakuwa vigumu kwao kuendelea kulima mazao hayo kwa wingi bila ya kuwa na uhakika wa soko.”

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo wa China alisema nchi yake iko tayari kutoa elimu na mafunzo kwa Watanzania hasa kwa kuandaa semina zitakazowawezesha washiriki kuongeza ujuzi wao, hatua ambayo itawasaidia Maafisa Ugani wetu kufanya kazi zao vizuri zaidi.
Katika mazungumzo hayo, Tanzania na China  zimesaini hati ya makubaliano ya  ushirikiano katika maeneo ya uvuvi, ambapo Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, Bw. Rashidi Ali Juma alitia saini kwa upanda wa Tanzania na China iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Eudong  Yu .
MapemaWaziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu Gavana wa Jimbo la Jiangsu, Bw. Guo  Yuan Qiang ambaye aliahidi kuwa jimbo lake litaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za elimu na afya. 
Gavana Qiang aliishukuru Tanzania kwa kuyawezesha makampuni kutoka jimbo  hilo ambayo yamejenga viwanda nchini na kufanya  shughuli zao kwa amani na usalama. 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 04, 2018

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post