Katikati ni Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Josephat Torner Foundation Europe,bwana Josephat Torner akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga. Kushoto ni Vedastus Wilfred,kulia ni Maria Msuva - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Jumla ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi 35 kutoka mataifa ya Ulaya na Afrika wanatarajia kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Septemba 21,2018 kwa ajili ya kuongeza uelewa wa jamii juu ya uwezo walio nao watu wenye ualbino katika jamii kufanya mbalimbali ya kijamii.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumanne Septemba 18,2018 katika Ofisi ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Josephat Torner Foundation Europe,bwana Josephat Torner amesema lengo la kupanda Mlima Kilimanjaro ni kuamsha uelewa wa jamii kuondokana na imani potofu za kishirikina juu ya watu wenye ualbino.
“Safari hii ya kupanda Mlima Kilimanjaro yenye Kauli mbiu ya “Vunja ukimya,Linda watu wenye ualbino” pia inalenga kutangaza utalii wa nchi ya Tanzania,tunaamini kuwa nchi yetu ya Tanzania itanufaika kwa kuendelea kuutangaza mlima wetu kimataifa na kupata fedha za kigeni”,alieleza Torner.
Aidha alisema baada ya shughuli ya kupanda mlima kwa muda wa siku nane, washiriki watatembelea mbuga ya wanyama Serengeti ili kujionea wanyama mbalimbali na mandhari nzuri ya mbuga hiyo.
“Pamoja na lengo kuu la kujenga uelewa wa jamii juu ya watu wenye ualbino,pia tutaitumia shughuli hii kama sehemu ya ugemaji rasilimali ambapo kila mshiriki atachangia dola za Kimarekani 1,000 na fedha hizo zitatumika katika kuwahudumia watoto wenye ualbino kwenye masuala ya elimu hasa wanaotoka katika kaya maskini”,alisema Torner.
“Nitoe wito kwa Umoja wa nchi za Afrika (AU) kuchukua hatua madhubuti kukomesha hali ya mauaji ya watu wenye ualbino yanayoendelea hivi sasa katika baadhi ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwa ni pamoja na Malawi,Msumbiji,Burundi,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Somali,Ghana,Rwanda na nchi nyinginezo”,aliongeza.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba waandishi wa habari kuendelea na moyo wa kujitoa katika kuripoti matukio ya unyanyasaji,mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino na watu wenye ulemavu kwa ujumla.
Taasisi ya Josephat Torner Foundation Europe (JTFE) yenye makao makuu nchini Uholanzi na nchini Tanzania ofisi zake zipo jijini Mwanza ina njozi ya kutengeneza jamii yenye amani inayojumuisha watu wote ambapo watu wenye ualbino watafurahia maisha yao bila hofu katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Na Kadama Malunde – Malunde1 blog
Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Josephat Torner Foundation Europe akielezea safari ya watu wenye ulemavu wa ngozi kutoka mataifa mbalimbali duniani kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Septemba 21,2018 - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Kushoto ni kijana Vedastus Wilfred mmoja wa washiriki wa upandaji Mlima Kilimanjaro akizungumza na waandishi wa habari leo.Wa Kwanza kulia ni Maria Msuva ambaye naye atapanda Mlima Kilimanjaro.