Serikali imesema kila aliyehusika katika shughuli ya kuokoa manusura na miili ya watu waliofariki katika ajali ya kupinduka kivuko cha MV Nyerere atapata kifuta jasho cha Sh400,000.
Mbali na kifuta jasho hicho, imeahidi kujenga wodi tatu za wanawake, wanaume na watoto katika Hospitali ya Bwisya wilaya Ukerewe jijini Mwanza pamoja na mnara wa kumbukumbu kwenye eneo la makaburi walipozikwa waliofariki katika ajali hiyo.
Fedha hizo zitakazotumika ni kati ya Sh946.6 milioni zilizokusanywa kama rambirambi kutokana na ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Septemba 20 na kupoteza maisha ya watu 228.
Akizungumza leo wakati wa kuhitimisha shughuli za uokoaji, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema maamuzi hayo ni kutokana na maagizo ya Rais John Magufuli.
Na Tumaini Msowoya, Mwananchi