Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WALALAMIKIA WAWEKEZAJI KUNG'OA MAZAO YAO JIRANI NA MGODI KATA YA NYAMTUKUZA KAKONKO

Wananchi wa kijiji cha Nyamwilonge kata ya Nyamtukuza wilayani Kakonko mkoani Kigoma wamewalalamikia wawekezaji wa  mgodi wa Nyamwilonge kwa kuwang'olea mazao yao yaliyoko jirani na mgodi huo kwa madai kuwa wanaingilia vitalu vyao.

Wakizungumza katika kikao cha kusikiliza na kutatua kero  katika Kijiji hicho leo kilichoandaliwa na uongozi wa kijiji na wilaya,  wananchi hao walisema  wawekezaji hao wamekuwa wakiwaonea na  wakikataa kuondoa mazao yao wamekuwa wakiwapeleka polisi.

Mmoja wa wananchi hao Emmanuel Katasheni alisema wao kama wananchi wanategemea kilimo ili kujikwamua na umaskini na kuzilea familia zao, hivyo kuiomba serikali kuwapatia  maeneo ya kufanyia kilimo.

Hata hivyo alisema wamekuwa wakionewa na wawekezaji hao kwa kuwatoza asilimia kubwa pindi wanapochimba katika mgodi wa wawekezaji hao, na wamekuwa wakiwanyonya na kusababisha mgogoro baina ya wachimbaji na wawekezaji.

Naye Michael Gasper ambaye pia ni mchimbaji mdogo, aliiomba serikali kuweka mipaka kwa wachimbaji waliopewa leseni ili na wao wajue maeneo ambayo yako wazi na waweze kuomba maeneo mengine na wao waweze kuchimba.

Aidha waliwalalamikia wawekezaji hao kutoshiriki katika mambo ya maendeleo kijijini hapo ikiwa ni pamoja na uchangiaji wa ujenzi wa vituo vya afya , shule na miradi mingine inayofanyiwa na wananchi. 

Kaimu Afisa madini  mkoa wa Kigoma, David Ndossy, alisema   hakuna mtu yeyote Tanzania mwenye ruhusa ya kuchimba madini bila kibali au leseni ya kuuza au kununua,  ambazo zinatolewa na Ofisi za madini mkoa na kila leseni inamalipo yake.

Alisema katika kijiji hicho wanawafahamu wachimbaji ambao wana leseni ni wawekezaji watano, hivyo wananchi wa kawaida ambao watahitaji kuchimba katika mgodi  huo lazima waingie makubaliano  na wawekezaji wenye leseni na watakao hitaji kuchimba.

Alisema ndani ya mita 200 kutoka katika eneo la machimbo hakutakiwi kuwa na shughuli za makazi wa kilimo zinazoendelea na wananchi waliopo katika eneo hilo wanatakiwa kuhama na kupewa maeneo mengine kwa ajili ya usalama wao kutokana na machimbo yaliyoanza tangu mwaka 2002 kuna maeneo mengi ambayo si salama kutokana na mashimo yaliyopo.


Alisema  masuala ya umiliki wa ardhi  yanaenda kisheria endapo eneo unaloishi lina madini serikali inatakiwa leseni  inampa umiliki wa kuchimba chini na unapokwenda kuchimba mahali na kuna watu wapo wanaishi muwekezaji anatakiwa kulipa fidia na kukubaliana na wananchi waweze kupatiwa maeneo mengine waweze kufanya shughuli nyingine.

"Kijiji kinajua ardhi yake na maeneo yake kwa hiyo madini hayahusiani na wamiliki wa ardhi endapo utakuwa eneo ambalo utamiliki kisheria kama lina madini  na kuhusiana na suala la mipaka wawekezaji wote ambao wamepatiwa leseni wanatakiwa kuweka mipaka yao na sheria inawataka hivyo",alisema.

Mmoja kati ya wawekezaji wanaolalamikiwa na wananchi kuhusu tuhuma ya kukamata watu na kuwaweka ndani na  kung'oa mazao ya wananchi, Jackson Mganyinzi aalisema asilimia kubwa  ya eneo linalochimbwa ni eneo lake  hajawahi  kutoza fedha nje na makubaliano ni asilimia 30% ya kile kilichopatikana kwa wachimbaji wadogo wa machimbo watakayochimba.

Alisema kuhusiana na suala la kuondoa mazao ya wananchi alifanya hivyo baada ya wananchi hao kupewa muda wa kuondoa mazao hayo na walipokaidi kuondoa mazao yao aliamua kung'oa mazao hayo.

Kufuatia malalamiko hayo mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala aliwataka wawekezaji na wananchi kuishi kwa mahusiano mazuri, na wasiwadhulumu wananchi pamoja na kuandaa mkataba utakaopitiwa na wanasheria ili wanaoingia kuchimba madini katika maeneo yao na wapatiwe risiti watakapolipa asilimi 3% ya madini wanayochimba na sio wawe wanadhulumiwa.

"Kuanzia sasa wananchi hawatalipa tena tozo ya kuchimba madini mpaka hapo utakapotengeneza mkataba unaotoa uhalali kwa wachimbaji wadogo na sio unyanyasaji na ninatoa wiki moja kwa wawekezaji wote kuondoa malalamiko lazima muandae mkataba unaoeleweka", alisema Kanali Ndagala. 

Alisema wawekezaji  lazima wawe wanatoa risiti ili kuweza kujua fedha zinazopatikana kupitia mgodi huo na kuweza kuchangia katika huduma za kijamii na kushiriki katika kutatua kero na kuinua uchumi wa kijiji kupitia  mgodi huo.

Sambamba na hayo alisema wawekezaji hao wanatakiwa kushiriki katika shughuli za maendeleo kama mwekezaji kujenga mahusiano mazuri ya kijiji na kuondoa ubabe wanaoufanya kwa kugomea kuchangia kijiji.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog


Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi - Picha na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com