Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA KILIMO DKT CHARLES TIZEBA AREJEA NCHINI BAADA YA KUMALIZIKA KONGAMANO LA AFRIKA LA MAPINDUZI YA KIJANI (AGRF 2018) NCHINI RWANDA

Kumalizika kwa Mkutano wa Mapinduzi ya kijani Barani Afrika (AGRF 2018) mjini Kigali nchini Rwanda kumeongeza tija na ufanisi kifikra kwa washiriki ikiwemo Tanzania kwa kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na mafanikio chanya kiuchumi kulingana na rasilimali zake nyingi za asili ikiwemo ardhi yenye rutuba katika kilimo.


Afrika ina hekta milioni 600 za ardhi isiyozalishwa ambayo ni sawa na asilimia 60 ya jumla ya kimataifa. Waziri wa kilimo Tanzania-Mhe Dkt Charles Tizeba anaamini kwamba mafanikio katika kukuza na kuimarisha uchumi Barani Afrika ni kupitia kilimo hivyo msisitizo mkubwa ni kusimamia kiufasaha mikakati inayowekwa kwenye sekta hiyo kuliko mijadala pekee.


Anasema Afrika inakadiriwa kuwa na idadi kubwa kufikia bilioni mbili mwaka wa 2030 hivyo mapinduzi ya kilimo yanapaswa kuimarisha mahusiano ya serikali na wananchi kwa kuwatunza wakulima kama wateja na kuwapatia ujuzi na huduma bora ili kuongeza uzalishaji wa Mazao yao.


Kurejea kwa waziri wa kilimo Mhe Tizeba jana tarehe 9 Septemba 2018 kunamfanya kuendelea na majukumu nchini mwake akiwa na fikra chanya kupitia tukio la kila mwaka la kongamano la Mapinduzi ya kijani (AGRF) linalowaweka pamoja wakuu wa nchi, wajasiriamali, wataalamu wa sekta na wakulima kwa mazungumzo muhimu juu ya hali ya kilimo barani Afrika.


Waziri huyo wa kilimo nchini Tanzania alipochangia mjadala kuhusu upotevu wa chakula baada ya uvunaji alisema jambo hilo limeendelea kuwa tatizo kubwa siyo tu katika chakula lakini pia katika malighafi kwa maendeleo ya viwanda huku akizitaja juhudi zilizofanywa na serikali ya Tanzania kupunguza upotevu wa chakula.


Dkt Tizeba, alielezea juhudi hizo kuwa ni pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, taasisi za kimataifa kama vile Bill and Melinda Gates foundation, HELVETAS Swiss Inter Cooperation Agency, Rockefeller foundation, AGRA, shirika la chakula Duniani, mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yameboresha kwa kiasi kikubwa teknolojia ya uhifadhi kama vile mifuko ya plastiki ya kuhifadhia nafaka ambayo imeonesha kuwa na mafanikio makubwa sana kwa kuzuia wadudu waharibifu kupenya na kushambulia nafaka.


Sambamba na hilo alisema juhudi za kupambana na upotevu wa chakula kumeifanya Tanzania kuanzisha mfumo wa kubadilishana bdhaa. Kuweka mazao katika masoko yaonekanayo ili kurahisisha uuzaji na kupunguza upoteaji wa bidhaa za kilimo. Chini ya mradi huu mazao yatatunzwa chini ya mfumo wa vikundi vya wakulima na kuuzwa moja kwa moja katika mfumo wa kupitia soko la bidhaa.


Kongamano hilo limefika ukomo hapo jana tarehe 8 Septemba 2018 baada ya kujadili maswala ya kilimo kwa siku nne mfululizo, lilihudhuriwa pia na viongozi wengine wa Afrika akiwemo Rais wa Ghana Mhe Nana Addo Dankwa Akufo Addo, Makamu wa Rais wa Kenya Mhe William Ruto, Waziri Mkuu wa Gabon Mhe Emmanuel Issoze-Ngondet sambamba na Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza Mhe Tony Blair.


Na Mathias Canal (WK), Dodoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com