Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA AKINAMAMA 100 WAJITOKEZA KATIKA ZOEZI LA UPIMAJI WA SARATANI YA MATITI


Dk Linda Malisa akiwafundisha akinamama waliofika katika uchunguzi wa awali wa Saratani ya matiti iliyotolewa bure na Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila (MAMC) ikiwa ni maadhimisho ya kuelekea mwaka mmoja wa kutoa huduma. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mmoja ya akinamama (mwenye blause nyekundu) akitoa ushuhuda kwa akinamama wenzake jinsi alivyoweza kuhudumiwa na kupatiwa vipimo na tiba ya saratani ya matiti. Uchunguzi wa awali wa Saratani ya matiti umetolewa bure na Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila (MAMC) ikiwa ni maadhimisho ya kuelekea mwaka mmoja wa kutoa huduma.

Dk Lilian Salingwa akimsikiliza mmoja ya akinamama aliyefika katika upimaji wa saratani ya matiti iliyoendeshwa na hospitali ya Rufaa Mloganzila (MAMC) ikiwa ni maadhimisho ya mwaka mmoja tokea imeanza kutoa huduma zake.
Dk Irona Elisante akitoa ushauri kwa mmoja wa akinamama aliyefika katika uchunguzi wa awali wa Saratani ya matiti iliyotolewa bure na Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila (MAMC) ikiwa ni maadhimisho ya kuelekea mwaka mmoja wa kutoa huduma.
Dk Mary Makuzola akitoa maelekezo kwa mmoja ya akinamama aliyefika katika uchunguzi wa awali wa Saratani ya matiti iliyotolewa bure na Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila (MAMC) ikiwa ni maadhimisho ya kuelekea mwaka mmoja wa kutoa huduma.
Daktari Bingwa wa kutafsiri picha za uchunguzi (Radiology), Dk Kiango akitoa maelekezo kwa mmoja ya akinamama waliojitokeza katika upimaji wa saratani ya matiti.

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila (MAMC) imeendesha zoezi la kuwapima bure akinamama ugonjwa wa Saratani ya Matiti.

Akielezea sababu ya kutoa huduma hiyo, Daktari Bingwa wa kutafsiri picha za uchunguzi (Radiology), Dk Lulu Sakafu alisema kuwa lengo la upimaji huo ni kuongeza uelewa wa magonjwa ya saratani ya matiti na kuadhimisha mwaka mmoja tangu taasisi hii kuanza kutoa huduma za afya.

Alisema mwito umekuwa mkubwa kwani zaidi ya wanawake 100 wamejitokeza kupata huduma hiyo na kati yao 30 wanadalili za saratani hivyo wameingizwa kwenye hatua ya uchunguzi ili kujua wangapi wana ugonjwa ili wapatiwe matibabu.

"Tangu kuanza kutoa huduma zetu tunatimiza mwaka sasa hivyo tuliangalia ni kitu gani cha kufanya kurudisha kwa jamii. Tukaone tufanye uchunguzi bure wa saratani ya matiti kwani wanawake wengi nchini wanakufa kwa sababu ya ugonjwa huo," alisema Dk Sakafu.

Pia alisema kuwa wanawake wanaowahi kupata matibabu ya saratani wanapona na hupata huduma hiyo kwa gharama nafuu ukilinganisha na wale wanaosubiri ugonjwa kufika hatua za mwishoni.

Dk Sakafu alisema wanatoa elimu ya jinsi ya kujichunguza wenyewe, kufanyiwa Ultrasound, mamografia na X-rays ambavyo vitachunguza uvimbe kwenye matiti.

Alifafanua kuwa dalili za saratani ya matiti ni uvimbe, ngozi ya titi kuwa na rangi ya chungwa, ziwa kuwa kubwa kuliko lingine na mtoke kwenye kwapa.

Kwa upande wake, Dk Linda Malisa alisema wanawake wengi wameutaja ugonjwa huo kuwa mwisho wake ni kifo, hofu na kwamba hakuna kitakachofanyika endapo utaumwa.

"Ugonjwa huu unatibika endapo utawahi kwenda hospitali kupata matibabu sahihi, tunaomba muwasikilize watu sahihi ambapo wamewekwa kwa ajili ya kutoa matibabu na sio mitaani ndio sababu wengi wanakufa kwa kusikiliza watu wasio sahihi," alisema Dk Malisa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com