Moja ya Matenki mapya ya Maji katika Mkoa wa Kusini Unguja yanayotowa huduma hiyo kwa Wananchi wa Wilaya ya Kusini Unguja.
Na. Abdi Shamna
Mamlaka ya Maji Zanzibar, (ZAWA), Wilaya Kusini Unguja, imeazimia kuyafanyia marekebisho makubwa matangi ya kuhifadhia maji yaliomo katika ameneo mbali mbali Wilayani humo, ili kufanikisha dhana ya upatikanaji wa huduma maji safi na salama kwa uhakika.
Hatua hiyo pia inatarajiwa kwenda sambamba na ya ubadilishaji wa mabomba ya kusafirishaji maji kutoka yale za zamani aina ya Asbestos (saruji) na kuweka ya mipira.
Hayo yameelezwa na Ofisa wa maji Wilaya ya Kusini Unguja, Hafidh Hassan Mwinyi katika mkutano uliopitia changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi wa Wilaya hiyo, kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi wake.
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Kusini Kitogani, umeratibiwa kwa mashirikiano kati ya Chama cha Waandishi Habari wanawake (TAMWA) Zanzibar, Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) pamoja na Jumuiya ya Uhifadhi wa msitu wa ngezi Pemba (NGERANECO).
Aidha, mkutano huo umewashirikisha Watendaji kutoka Serikali za Mitaa Wilaya Kusini Unguja, Waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali pamoja na CSO.
Akizungumza na wadau hao, Mwinyi alisema malengo hayo ya muda mrefu yatahusisha ubadilishaji wa matangi kadhaa ya kuhifadhia maji Wilayani humo, kutoka yale yaliopo hivi sasa aina ya Sandarusi na kuweka ya vyuma.
Alisema hatua hiyo inatokana na matangi mengi yaliopo hivi sasa kuwa na uwezo mdogo wa kuhifadhi maji kutokana na uchakavu.
Aidha ,alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa muongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lililopiga marufuku matumizi ya mabomba ya Asbestos, kwa maelezo ya kusababisha ugonjwa wa cancer.
“Kuna mabomba ya Asbestors katika baadhi ya maeneo, ni hatari na husababisha magonjwa ya canser, pamoja na WHO kupiga marufuku matumizi ya mabomba hayo, lakini bado Zanzibar yanatumika katika baadhi ya maeneo’, alisema.
Alisema pamoja na juhudi kadhaa zinazochukuliwa na Serikali za kuhakikishia Mamlaka hiyo inawafikishia wananchi wake huduma hiyo muhimu, bado kuna changamoto mbalimbali, nyingine zikisababishwa na wananchi, ikiwemo matumizi yasio sahihi ya maji safi na salama.
Alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu kwa uhakika na kubainisha kuwepo kwa matumizi makubwa ya maji kwa shughuli za kilimo, jambo ambalo haliniendani na azma hiyo.
Alisema matumizi ya maji kwa shughuli za kilimo cha migomba unaofanywa na baadhi ya wakaazi wa shehiya za Makunduchi, kunadhoofisha juhudi za ZAWA za kuwafikishia huduma hiyo wananchi.
Alibainisha kuwa ZAWA imejipanga kuweka utaratibu maalum, ikiwa pamoja na kufunga mita kwa wananchi wote wanaotumia maji kwa shughuli za kilimo, ikiwa ni hatua ya kudhibiti upotevu mkubwa wa maji na fedha za umma.
Katika hatau nyengine, Ofisa huyo alieleza hatari inayowakabili wananchi wa shehiya mbali mbali za Wilaya hiyo ya kukosa huduma za maji baridi, baada ya visima vingi kubainika kukumbwa na tatizo la kuingiliwa na maji chumvi, ambapo moja ay sababu zake ni ufungajj wa mabomba makubwa.
Mradi wa Kukuza Uwajibikaji, ulio chini ya usimamizi wa ZANSAP na Ufadhili wa Jumuiya Ulaya (EU), unatekelezwa katika Wilaya zote 13 za Unguja na Pemba.
Aidha umewashirikisha Watendaji wa Serikali za Mitaa, Waandishi wa habari na CSO.