Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza kuwa kamata na kuwachukulia hatua wale wote wanaoendesha makundi ya ngono na wanaoweka picha za uchi na kujiuza kwenye mitandaoni ya kijamii.
Akizungumza na EATV Saa 1 leo jijini Dar es salaam, Joshua Mwangasa ambaye ni Mrakibu msaidizi wa jeshi la Polisi nchini, kutoka kitengo cha uhalifu wa mtandao amesema wanaendelea na uchunguzi wa kuwabaini wale wote wanaoendesha biashara ya kujiuza na kuweka picha za uchi kwenye mitandao ya kijamii hususan kwenye Whatsapp na Instagram.
Ameiambia EATV Saa1 kuwa tayari watu kadhaa wamekamatwa na wanaendelea kuhakikisha kuwa wanawabaini wote, kwani kujiuza na kuweka picha za uchi ni kosa la jinai kupitia sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015.
Amesema, Sheria hiyo pia inapiga marufuku mtu yeyote kuweka mtandaoni video au picha inayoonyesha ukatili wa kingono kwa watoto, hivyo yeyote atakaye tenda makosa hayo na kubainika mara moja atashikiliwa na jeshi hilo.
Mapema mwezi Septemba, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alitoa onyo kwa wasanii nchini kuacha kutumia vibaya mitandao ya kijamii na endapo hatofanya hivyo basi watachukuliwa sheria stahiki dhidi yao.
Ambapo Septemba 21, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Faidha Omary maarufu kama Sister Fey alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa kosa la kukiuka maadili kwa kuchapisha maudhui yanayodhalilisha kwenye mitandao ya kijamii kwa amri ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
CHANZO - EATV
Social Plugin