Watu watatu wamepoteza maisha na wengine sita kujeruhiwa, baada ya gari walilokuwa wakisafiria linalomilikiwa na wakala wa barabara nchini (Tanroads ) mkoa wa Kagera, kugongwa na gari la mizigo na kisha kuangukia kwenye moto na kuteketea.
Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi alisema ajali hiyo imetokea Oktoba 23 mwaka huu saa saba na nusu mchana katika eneo la Mushasha wilayani Missenyi, wakati gari la Tanroads likitokea wilayani Ngara kuelekea Bukoba na gari la mizigo likitokea Bukoba kuelekea Uganda.
Kamanda Malimi alitaja majina ya waliopoteza maisha kuwa ni David Dickson (25), Pavin Ibrahimu (28) na Hamad Abdul (25) wote vibarua wa Tanroads.
Alitaja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Leah Mussa (32), Happiness Geofrey (30), Zamda Salehe (28) Dorine Mbatina (31) wote vibarua wa Tanroads, Salum Chomba (50) mfanyakazi wa Tanroads na Greyson Rwegasira (40) dereva wa Tanroads.
Alisema kuwa gari la mizigo lilikuwa likiendeshwa na Patrick Shabieri (43) mzaliwa wa Bukavu nchini Kongo, na kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva wote wawili.
“Eneo ilikotokea ajali kulikuwa na moto ukiwaka, madereva wote hawakuchukua tahadhali wakati kulikuwa na moshi uliotokana na moto huo, gari la Tanroads liligongwa likaangukia kwenye moto na kulipuka” ,alisema.
Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Kagera Nelson Lumbeli amekiri kupokea miili mitatu na majeruhi sita wakiwamo wanawake wanne na wanaume wawili, na kuwa mmoja kati yao hali yake siyo nzuri.
“Kuna majeruhi anaitwa Leah Mussa hali yake siyo nzuri sana kwa sababu kwa mujibu wa madaktari mwili wake umeungua kwa asilimia 75, lakini hawa wengine hali zao zinaendelea vizuri na kama wataendelea hivi wataweza kuruhusiwa”, alisema.
Kwa upande wake meneja wa Tanroads mkoani Kagera, mhandisi Andrea Kasamwa, alisema kuwa amepoteza wafanyakazi wake waliokuwa katika majukumu ya kulitumikia taifa, na kutaja idadi ya wafanyakazi waliokuwa katika gari hilo kuwa ni tisa.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo Dorine Mbatina alisema kuwa walipofika eneo la ajali kulikuwa na moto na moshi uliokuwa ukisababisha madereva wasione mbele vizuri, na ghafla waliona gari la mizigo likuwa limewakaribia na kugonga gari lao.
“Baada ya kugongwa gari letu lilibiringika mara tatu na kudondokea katika moto, vioo vilipasuka na sisi wengine tukabahatika kupita katika vioo vilivyopasuka, lakini gari likalipuka moto mkali na wengine waliopoteza maisha wakashindwa kutoka” alisema.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Kagera, waliopoteza maisha katika ajali hiyo miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa, iliyoko katika manispaa ya Bukoba.
Na Mwandishi wa Malunde1 blog