Watu 42 wamekufa kutokana na ajali baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Nairobi kwenda Kisumu kupinduka eneo la Fort Ternan katika barabara Londiani-Muhuroni, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kericho James Mogera amethibitisha.
Basi hilo lenye viti 67 inasemekana lilibadili uelekeo na kutoka nje ya barabara lilipokuwa linashuka kwenye mteremko. Basi liligonga ukingo kisha likapinduka na kutumbukia kwenye korongo la urefu wa mita 20.
Mashuhuda wanasema kwamba ajali hiyo imetokea alfajiri ya saa 11:00 Jumatano.
Mogera alisema idadi ya watu waliopoteza maisha inaweza kuongezeka kwa kuwa wengi walikuwa bado wamefunikwa chini.
Majeruhi wamechukuliwa na kupelekwa zahanati ya Fort Ternan na Hospitali ya Muhoroni kwa matibabu.
Miongoni mwa waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo ni watoto watano wa umri chini ya miaka mitano.
Shuhuda mmoja, Jackson Koskei, ameliambia gazeti la Nation kwamba alisikia honi ikipiga kwa muda mrefu kisha kishindo ambacho punde kilifuatiwa na kelele za abiria waliokuwa wakilia kwa sauti.
Via>>Mwananchi
Social Plugin