Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ALIWA NA MAMBA AKIOGELEA ZIWANI

Mkazi wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Msema Msafiri maarufu kwa jina la Giriki (35), ameliwa na mamba, alipokwenda katika mwambao wa Ziwa Tanganyika kuogelea.


Imeelezwa kuwa Msafiri, mkazi wa Kitongoji cha Lyela kilichopo mwambao wa Ziwa Tanganyika katika Kijiji cha Izinga Kata ya Wampembe, alikwenda kuogelea kutokana na joto kali alilokuwa akilihisi.


Alikumbwa na mkasa huo Ijumaa majira ya mchana, baada ya kuingia ziwani na kuanza kuogelea.


Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Izinga, George Fataki, alisema kuwa kijana huyo alikuwa ni mgeni katika kitongoji hicho na alikuwa ametokea mkoani Kigoma katika Kijiji cha Kalago na kwenda katika katika kitongoji hicho ambacho ni makazi ya wavuvi mwezi mmoja uliopita, kwa lengo la kufanya shughuli hizo.


Alisema kwa kuwa mazingira aliyotoka yalikuwa na baridi, hivyo mazingira ya ziwani yalikuwa yakimsumbua kutokana na joto kali, kitendo kilichosababisha ajenge mazoea ya kwenda kuogelea ziwani.


Kwa mujibu wa Fataki, siku ya tukio hilo majira ya saa 8 mchana aliwaaga wavuvi wenzake kuwa anakwenda kuupoza mwili kwa kuogelea ziwani na alipofika aliingia ndani ya maji na kuanza kuogelea, ghafla aliibuka mamba na kumvutia katika kina kirefu cha maji na kuanza kumla kisha kuondoka naye.


Mwenyekiti wa kijiji hicho alisema kuwa baadhi ya wavuvi walikuwa wanashuhudia tukio hilo kwa mbali, lakini walishindwa kutoa msaada, hivyo mamba huyo kuondoka na Msafiri na mpaka sasa jitihada za kuutafuta mwili wake zinaendelea.


Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwatahadharisha wananchi wanaoishi maeneo ya mwambao mwa ziwa na mito kuacha tabia ya kwenda kuogelea, kwa kuwa ni hatari kwa usalama wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com