Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeruhusiwa kurejea katika Shirikisho la Mashirika ya Ndege Duniani (IATA), ambapo kuanzia sasa litakuwa na uwezo wa kuuza tiketi zake duniani kote.
ATCL iliondolewa IATA miaka tisa iliyopita baada ya kuelemewa na mzigo wa madeni.
Lakini tangu kufufuliwa upya kwa shirika hilo 2016, limekuwa likipambana kutaka kurejea upya katika uanachama ili kuepuka kukosa malipo ya tiketi zao hususan katika safari za kimataifa.
Taarifa ya ATCL iliyotolewa kwa washirika wake Oktoba 24 na kuthibitishwa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Ladislaus Matindi jana kwa ujumbe mfupi wa simu kwa Mwananchi inaeleza kuwa, kurejeshwa kwao kumeanza rasmi mwezi huu.
“Tulipata taarifa kutoka IATA kuwa tumerudishwa kwenye mfumo wa malipo wa pamoja (Airlines Clearing House - ACH)), na sasa Air Tanzania imerejea katika mfumo huo na ni mwanachama halali wa shirikisho hilo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na mkurugenzi wa Fedha, Albinus Manambu.
Via Mwananchi
Na Ephrahim Bahemu, Mwananchi