Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ATUPWA JELA MIAKA 5 KWA KOSA LA KUKUTWA NA MADINI BILA LESENI

Mfanyabiashara  Hafidhi Jonggradgorn ametiwa hatiani na madini yake yenye thamani ya Dola za Marekani 105,757.38 kutaifishwa na Serikali baada ya kukiri kosa la kukutwa na madini hayo bila leseni.

Mshtakiwa huyo alihukumiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Mahakama hiyo ilimtia hatiani na kumhukumu kwenda jela miaka miwili au kulipa faini Sh milioni mbili kwa kosa la kwanza na kosa la pili jela miaka mitatu au faini Sh milioni tatu.

Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori alimkumbusha mshtakiwa mashtaka yanayomkabili ambapo alidai anadaiwa kutenda kosa kati ya Januari 2017 na Juni 3, 2018.

Nyantori alidai shtaka la kwanza mshtakiwa anadaiwa katika maeneo tofauti Tanzania na Falme za Kiarabu na India, akiwa si mtumishi wa umma kwa makusudi alifadhili biashara ya madini kwa lengo la kupata faida.

Nyantori alidai katika shtaka la pili, mshtakiwa katika tarehe hizo maeneo ya Mikocheni A, Mtaa wa Chwaku alikutwa na vito vya thamani aina ya gamestones kilo 62.76 vyenye thamani ya Dola za Marekani 105,757.38.

Mshtakiwa alikiri makosa hayo na kutiwa hatiani na upande wa mashtaka ulitaka apewe adhabu kwa mujibu wa sheria kwa sababu mshtakiwa ameingilia maliasili za taifa.

“Mheshimiwa Hakimu tunaomba madini yataifishwe yakabidhiwe serikalini chini ya Tume ya Madini, bastola arejeshewe mshtakiwa,” alisema Nyantori.

Akijitetea mbele ya hakimu, mshtakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwani ana familia na watoto wameshindwa kwenda shule kwa sababu ya kukosa ada, ni mfanyabiashara anayeipa Serikali kipato.

Hakimu Mashauri alisema mshtakiwa mbinu anayotumia inaikosesha Serikali mapato, hivyo alimuhukumu kwa kosa la kwanza faini Sh milioni mbili au kwenda jela miaka miwili.

Alisema kosa la pili faini Sh milioni tatu au jela miaka mitatu.

Hata hivyo mshtakiwa hajalipa faini hivyo amekwenda jela.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com