Mzee anayenufaika na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Tasaf, Anthony Mikami (76) amejinyonga kwa kamba ya chandarua katika kijiji cha Nyabihanga kata ya Bukiriro wilaya ya Ngara mkoani Kagera kwa kile kinachodaiwa kuwa na msongo wa mawazo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyabihanga, Eradius Batakanwa amesema mzee huyo alijinyonga kwa kujitundika kamba kwenye mti mbali na makazi ya watu na aligundulika jana Jumatano Oktoba 24, 2018 saa 9:30 mchana kwa waliokwenda mabondeni kuvuna maharage.
Batakanwa amesema siku za hivi karibuni wakati wa uhai wake akiwa mnufaika wa Tasaf kijijini humo aliunguliwa na nyumba wakati akichoma viroboto na kuiteketeza nyumba hiyo.
"Baada ya kuunguliwa nyumba alichanganyikiwa maana alikuwa hana chakula cha usiku na mchana huku akiwa hana wasaidizi licha ya kujaliwa watoto watano wa kiume mmoja na wakike wanne," amesema Batakanwa na kuongeza kuwa hilo ni tukio la pili baada ya lile la kwanza lililotokea Februari.
Batakanwa pia amewataka watu wenye msongo wa mawazo kutafuta ushauri kwa viongozi wa dini ili kuepuka kujiondoa uhai wao.
Mkuu wa kituo kidogo cha polisi kata ya Bugarama, Dotto Baraka na mganga mfawidhi wa kituo cha Afya Bukiriro, Themistocles Rubangula wamethibitisha kifo cha mzee huyo.