Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BALOZI WA KENYA AFANYA ZIARA SIMIYU KUJIONEA FURSA ZA UWEKEZAJI


Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akimkabidhi Nakala ya Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu, wakati wa ziara yake mkoani humo, Oktoba 03, 2018.
Kutoka kulia Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini, Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu na Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery kilichopo Bariadi, Bw. Boaz Ogola wakiteta jambo, wakati wa ziara ya Balozi huyo mkoani Simiyu, Oktoba 03, 2018.
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu , Mjini Bariadi wakati wa ziara yake mkoani humo, Oktoba 03, 2018.
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu ( wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mkoa wa Simiyu mara baada ya kuhitimisha ziara yake mkoani Simiyu, Oktoba 03, 2018.
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu akisalimiana na Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka(kulia) , mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi wakati wa ziara yake mkoani humo, Oktoba 03, 2018.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka(kulia) akisalimiana na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu, mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi wakati wa ziara yake mkoani Simiyu, Oktoba 03, 2018.
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu, akisalimiana na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi wakati wa ziara yake mkoani Simiyu, Oktoba 03, 2018.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu amefanya ziara mkoani Simiyu Oktoba 03, 2018 na kuzungumza na viongozi wa mkoa huo, ambapo ameeleza kuwa moja ya malengo ya ziara yake ni kufahamu Mipango na Fursa za Uwekezaji zilizopo mkoani Simiyu, ili aweze kuzungumza na wawekezaji nchini Kenya kuwekeza mkoani humo.

Balozi Kazungu amesema nchi ya Kenya ndiyo inaongoza kuwekeza nchini Tanzania ukilinganishwa na nchi nyingine za Afrika ambapo hadi sasa imewekeza takribani dola za Kimarekani bilioni 1.6 hapa nchini.“ Nimekuja hapa ili tufahamiane vizuri, nijue mipangilio yenu, fursa za uwekezaji ziko wapi ili tuweze kuzungumzana wenzetu wakaja kuwekeza, Kenya ni nchi inayoongoza kwa kuwekeza nchini Tanzania, hadi sasa imewekeza takribani dola bilioni 1.6 ”, alisema Balozi Kazungu.

Aidha, ameomba ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uendelee kuimarishwa kwa lengo la kuzifanya nchi hizi kuwa shina la viwanda na uwekezaji na kuwa wanufaika wa soko la pamoja la Afrika hali itakayochangia kuimarisha uchumi wa nchi hizo.Pamoja na ushirikiano katika masuala ya uwekezaji na viwanda Balozi Kazungu amesisitiza masuala ya ujirani mwema, upendo na ushirikiano wa kindugu baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo inakaribisha sekta binafsi na iko tayari kutoa ardhi bure kwa wawekezaji walio tayari kuwekeza Simiyu katika maeneo yanayojibu mahitaji ya mkoa na nchi kupitia malighafi zinazolishwa ndani ya mkoa na ndani ya nchi.

“Kwa mtu aliye tayari kujenga kiwanda kinachojibu mahitaji yetu kama mkoa hasa kitakachutumia malighafi tulizonazo mfano atakayewekeza kwenye viwanda vya kusindika nyama, viwanda vya kutengeneza bidhaa za ngozi, pamba na yeyote atakayewekeza kwenye viwanda vyenye malighafi inayozalishwa hapa nchini, tutampa ardhi bure”, alisema.

Mtaka amemweleza Balozi Kazungu kuwa mkoa huo pia uko tayari kutoa ardhi bure kwa wawekezaji walio tayari kuwekeza kwenye ujenzi wa vyuo ikiwemo vya ufundi na utalii ili kuwajengea vijana ujuzi.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema mafanikio ya Mkoa huo yanayopelekea kufanya vitu vikaonekana ikiwa ni pamoja na kuwa na Mwongozo wa Uwekezaji ni ushirikiano uliopo kati ya viongozi, watendaji, wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwepo Taasisi za Serikali na binafsi, sekta binafsi, madhehebu ya dini pamoja na wananchi.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery kilicjopo Bariadi, Bw. Boaz Ogola ambaye ni Mwekezaji kutoka nchini Kenya amemweleza Balozi kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na mahali sahihi kwa uwekezaji, hivyo akatoa wito kwa Mhe. Balozi kuwaalika Wafanyabiashara kutoka Kenya kuja kuwekeza Simiyu na Tanzania kwa ujumla.
Na Stella Kalinga, Simiyu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com