Daktari feki anayefahamika kwa jina la Joseph Samwel (26),amekamatwa katika Hospitali ya Rufani ya Bugando mkoani Mwanza, baada ya kutafutwa takriban mwezi mmoja kutokana na malalamiko ya wagonjwa.
Wagonjwa na watu mbalimbali wanaofika hospitalini hapo wamekuwa wakilalamika kutapeliwa fedha na watu wanaojitambulisha kwao kuwa ni watumishi wa hospitali hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Abel Makubi, Ofisa Uhusiano wa Hospitali hiyo, Lucy Mogele, alisema uongozi ulifanya jitihada za kufuatilia malalamiko hayo kwa kuweka mitego kadhaa, ambayo ilifanikisha kumkamata mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
"Joseph amekuwa akijitambulisha kwa nafasi mbalimbali kama daktari, muuguzi na mwanafunzi wa udaktari na baada ya jitihada kufanyika, daktari huyo feki alikamatwa Oktoba 3, mwaka huu, majira ya saa moja jioni ndani ya eneo la hospitali kwa msaada wa wauguzi na madaktari, "alisema Mogele.
Kwa mujibu wa Mogele, katika maelezo yake, Joseph alidai kuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa shahada ya uuguzi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino kilichoko jijini Dodoma.
"Kimsingi kozi hiyo haipo katika mitaala ya kitabibu na chuo kilichotajwa hakiko jijini Dodoma," alisema.
Katika mahojiano ya uongozi wa hospitali hiyo, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na matukio mengi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wagonjwa huku akiwaahidi kuwapatia huduma.
"Kijana huyu amekuwa akizungukia sana maeneo ya wodini na hata wagonjwa wenyewe wamekiri kuwa alikuwa akiwatapeli. Watu kama hawa wamekuwa wakisumbua wagonjwa, ikiwamo upotevu wa vitu na fedha zao na kuwapatia huduma ambazo si sahihi," alisema Mogele.
Naye Mwanasheria wa hospitali hiyo, Anacket Kamara, alitoa wito kwa wananchi wote wanaofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kutibiwa, kufuata taratibu za matibabu zilizowekwa na uongozi.
Alisema kama kuna mahitaji ya kupata ufafanuzi au maelekezo na ushauri, watumie dawati la maulizo au kuonana na watumishi wenye sare za ‘niulize nikusidie’ au wapige simu zilizoko katika mbao za matangazo.
"Ni haki ya kila mwananchi kuomba kuona kitambulisho cha mtoa huduma katika eneo husika ili kuepukana na madaktari feki ambao wanachukua fedha na kushindwa kuwahudumia na kusababisha malalamiko na mtuhumia Joseph yuko chini ya ulinzi akisubiri sheria ichukue mkondo wake," alisema Kamara.
Social Plugin