Mwanafunzi Ndemezo Lutakwa ambaye ameshika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba 2018 yaliyotangazwa jana amesema kuwa maandalizi mazuri ya walimu kimasomo, nidhamu na kupenda masomo ndiyo yaliyomfanya aweze kufaulu vizuri mitihani yake.
Mwanafunzi huyo aliyehitimu elimu yake ya msingi katika Shule ya Kadama English Medium iliyopo Kata ya Buseresere wilayani Chato mkoani Geita ameyasema hayo kijijini kwao Igando, Magenge wilayani Geita.
Baba Mzazi wa mwanafunzi aliyeibuka kinara (Tanzania one) kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu, Ndemezo Rutakwa Lubonankede kwenye matokeo ya mitihani ya darasa la saba ambaye anafahamika kama Rutakwa Rubonankede amesema licha ya kijana wake kuibuka kinara wa darasa la saba lakini yeye mwenyewe hakusoma hata darasa moja.
Mwanafunzi wa kwanza kitaifa matokeo la saba Ndemezo Rutakwa.
Mzee Rutakwa Lubonankede amesema alishindwa kusoma kutokana na hali ya nyumbani kwao ambapo baba yake alimlazimisha kuacha shule ili kusaidia kazi za nyumbani.
“Kiukweli mimi sikusoma hata darasa moja kwa hiyo sababu kubwa ilikua baba yangu alikuwa mzee sana, nilipopata mtoto nilitamani awe msomi kama wasomi wengine, ndio nikaamua kupeleka wanafunzi watatu pale”, amesema Rutakwa Rubonankede.
Aidha mzee Rutakwa Rubonankede amesema juhudi za mtoto wake aliziona tangu alivyokuwa mdogo kutokana na namna anavyopangilia ratiba pamoja na kujituma kwenye masuala ya masomo.
“Kilichomuwezesha ni kujituma na kila kazi alikuwa anaipenda na mimi nilikuwa nampongeza sana, ndio maana imemuwezesha kufanya vizuri kwenye masomo yake", ameongeza.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa Charles Msonde alitangaza matokeo ya darasa la saba jana Jumanne, ambapo katika orodha ya wanafunzi ya waliofanya vizuri Ndemezo Rutakwa kutoka shule ya msingi Kadama mkoani Geita alitangazwa kuwa wa kwanza kitaifa.
Kutazama matokeo hayo
Chanzo -AZAM TV