Serikali Wilayani Chunya imesema haitawafumbia macho wala kuwachekea baadhi ya wafugaji ambao watabainika kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi MaryPrisca Mahundi, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Upendo, Kata ya Kipembawe Wilayani Chunya.
Alisema asilimia kubwa ya malalamiko katika kijiji hicho ni juu ya wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima tena kwa maksudi hivyo akiwa kama kiongozi wa Wilaya hiyo hatavumilia kuona uharibifu huo ukifanyika.
“Nataka kufahamu hichi kiburi cha wafugaji jamii ya kisukuma mnakitoa wapi, lakini eleweni kwamba nitawashughulikia na mtaomba kuhama kwenye kijiji hiki hata kama mnatembea na fimbo na silaha lakini mtahama endapo hamtajirekebisha.
Akizungumzia suala la ubakaji na mauaji yanayotokana na imani za kishirikina, Mkuu huyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwabaini watu wenye tabia za kubaka, kulawiti na wanaofanya mauaji ya watu wasio na hatia kwa kisingizio cha imani za kishirikina.
“Mwanaume una miaka 35 unaenda kumbaka mtoto wa miaka mitatu, wewe si mtu wa kawaida ni mnyama, hivyo tunataka hii tabia ikome,mnadanganyana kwamba ukimbaka au kumlawiti mtoto basi utakuwa tajiri kwa kupata mazao mengi shambani au madini kwenye machimbo, jambo hili halivumiliki wakati umefika kwa watu hawa kukomeshwa,”alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi MaryPrisca Mahundi, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Upendo, Kata ya Kipembawe Wilayani Chunya.
Wananchi wa kijiji cha Upendo, Kata ya Kipembawe Wilayani Chunya wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi MaryPrisca Mahundi
Social Plugin