Gullam Hussein Dewji, baba wa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ amesema Sh1 bilioni ambazo familia yake iliahidi kumpatia mtu ambaye angefanikisha kupatikana kwa mwanaye hazitatolewa.
Akizungumza na Mwananchi jana Gullam alisema hakuna aliyefanikiwa kupata fedha hizo kwa kuwa Mo alipoachiwa na watekaji, ni yeye mwenyewe ambaye aliomba msaada wa simu katika Hoteli ya Southern Sun jijini hapa.
Alisema hakuna aliyewasiliana na familia hiyo na kutoa maelezo yaliyosaidia kupatikana kwake.
“Ndugu yangu hiyo zawadi kama nilivyokwambia simu alipiga Mohammed mwenyewe akinipigia mimi sio kwamba mtu alinipigia akaniambia kwamba mwanangu yuko wapi,” alisisitiza.
Kuhusu afya ya mwanaye alisema, “Mohamed anaendelea vizuri mpaka sasa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kweli. Unajua sisi kama familia hatuwezi kusema zaidi mambo ya kiuchunguzi yapo chini ya Jeshi la Polisi wao ndiyo wenye mamlaka hayo.”
Lakini wakati Gullam akisema hakuna anayestahili Sh1 bilioni kwa kuwa hakuna aliyetoa taarifa zilizowezesha kupatikana kwa mtoto wake, jana mchungaji wa mitume, manabii na maaskofu Tanzania wa Kanisa la Emmaus Bible Church Pentecostal lililopo Mbezi Kibanda cha Mkaa, Dar es Salaam, Komando Mashimo alisema anapaswa kupewa yeye.
Akizungumza katika ibada ya kumshuruku Mungu baada ya kupatikana kwa bilionea huyo alisema, “Naweza kusema hiyo fedha ni yangu kama ataamua kutoa maana nimetabiri ataonekana na ameonekana. Ikitokea amekubali kunipa nitamuomba anijengee kanisa.”
Social Plugin