Shamba lililopandwa mbegu chotara lililoliwa na wadudu bungua na viwavijeshi
Na Hellen Kwavava
Uelewa Mdogo na Hofu ya Jamii kuhusu Teknolojia ya Uhandisi Jeni(GMO) ndiyo kikwazo kikubwa cha kusababisha Teknolojia hii kutofika kwa wakulima kwa haraka.
Miaka ya hivi karibuni tabia ya nchi imehatarisha maisha kwa wakulima kwani hali ya ukame imetokea jambo linalosababisha ulimaji wa mazao mbalimbali kushuka pamoja na kukumbwa na magonjwa kiasi ambacho uzalishaji kuwa mdogo na kusababisha njaa kwa jamii pamoja na uchumi kwa wakulima wengi kushuka.
Kwa muda sasa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia majukwaa mbalimbali yakiwemo Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo Tanzania(OFAB) pamoja na wadau mbalimbali wa kilimo imekuwa ikifanya jitihada kuelimisha wananchi kuhusiana na faida za kutumia teknolojia ya uhandisi Jeni.
COSTECH inafanya hivi kwa kuwa imepewa mamlaka na Sheria No 7 ya Bunge ya Mwaka 1986 kuratibu na kuendeleza tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Pamoja na jitihada hizi za COSTECH na wadau wengine wa kilimo, changamoto inaonekana ni kubwa sana hususani kwa baadhi ya vikundi kupotosha maana halisi ya teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) kwamba teknolojia hii ina madhara kwa afya ya Binadamu.
Akizungumza mkoani Dodoma Kwenye Shamba la majaribio la Mahindi yaliyowekewa Vinasaba (MAKUTUPORA) Mshauri wa Ofab Tanzania Dkt Nicolaus Nyange alisema kuna hoja ambazo hazina mashiko ya kitafiti wala kisayansi tu.
“Watu wanasema Teknolojia hii ina madhara lakini inaonekana kuna upinzani wa kibiashara,upinzani kuhusu Teknolojia hii ya Uhandisi Jeni hutolewa kutokana na sababu za kibiashara za kuhofia teknolojia hii inaweza kuua soko la viwanda mbalimbali hususani vile vya Pembejeo”,alisema Dk. Nyange.
Teknolojia hii imekwishafanyiwa tafiti za kutosha na wataalamu wetu nchini wakiwemo wale wa Taasisi ya Kilimo ya Mikocheni pamoja na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Makutupora(TARI) ambapo Dkt. Justin Ringo mgunduzi Mkuu wa Mbegu Mahindi iliyowekewa Vinasaba alisema Uhandisi Jeni ni teknolojia nzuri ambayo kama tutaitumia vizuri inaweza kuharakisha zaidi maendeleo ya kilimo chetu na hatimaye kutusaidia katika mapinduzi makubwa ya viwanda na uchumi wa nchi yetu.
“Unajua uhandisi Jeni ni hali ya kupandikiza DNA ya kirusi cha Ugonjwa flani unaoathiri mmea katika mmea husika ili kujenga kinga ya mmea huo ambapo Mbegu za mazao ambazo zimefanyiwa uhandisi Jeni zina kinga ambayo hustahimili magonjwa hivyo mkulima anaweza asitumie kabisa mbolea”,alisema Dk. Ringo
Utafiti unaofanywa kuhusiana na Teknolojia hii unaonyesha kufikia lengo kwa Asilimia 100 ambapo inauwezo wa kuhimili ukame pamoja na wadudu vamizi wa mazao ambao wamekuwa kero kubwa na hasara kwa wakulima na jamii kwa ujumla.
Social Plugin