Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ alitekwa jana alfajiri Oktoba 11, 2018 jijini Dar es Salaam kwenye Hoteli yaColosseum iliyopo Oysterbay alipokwenda kwa lengo la kufanya mazoezi.
Akizungumzia tukio hilo jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema katika uchunguzi wao wa awali kupitia kamera za ulinzi (CCTV) zimeonyesha magari mawili yalihusika.
Mambosasa amesema katika tukio hilo magari hayo mawili yalifika hotelini hapo kabla MO hajafika.
Amesema gari ya kwanza aina ya Toyota Surf ilikuwa imeegeshwa nje ya geti la kuingilia hotelini likiangalia usawa wa ndani ya hoteli, huku la pili aina ya Toyota Noah likiegeshwa pembeni kidogo ya eneo ambalo MO hupaki gari lake kila afikapo hotelini na kushuka.
Wakati Mo akifika hapo kamera zilionyesha gari ya ndani aina ya Noah ikiiwashia taa gari ya nje kuashiria kwamba Mo amefika.
Mara baada ya kuwasha taa hizo wakati Mo anashuka watu wawili raia wa kigeni (Wazungu) waliteremka na kuingia ndani ya geti la kuingilia kisha kukutana na Mo akiwa anafunga gari yake na kuanza kuingia ndani ya jengo.
Watu hao wawili walifika kwa Mo na kufanikiwa kumbana vizuri ambapo wakati wakiendelea na kazi hiyo gari iliyopaki nje ilikuwa imeshafanikiwa kuingia ndani ya geti na watekaji kufanikiwa kumuingiza katika gari iliyotoka nje aina ya Surf.
Mara baada ya watekaji kufanikiwa walimpokonya funguo ya gari na simu yake kisha kuzitupa chini na kuanza safari ya kuondoka eneo hilo.
Kamera zilionyesha tukio hilo lilikamilika majira ya saa 11:35 alfajiri ambapo wakati wanatoka, Surf ambayo ilimbeba Mo ilitangulia mbele huku Noah ikifuata nyuma mpaka kwenye geti la kutokea.
Walipofika hotelini hapo Wazungu hao, alishuka mmoja na kufyatua risasi mbili juu kuamrisha mlinzi afungue geti ambapo wakati walinzi wakijisalimisha Mzungu aliyeshuka akakimbia getini na kufungua geti mwenyewe na gari zote kufanikiwa kukimbia.
Social Plugin