Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni mbunge wa CHADEMA, Godbless Lema amesema njia pekee ya Serikali kujiondoa katika lawama tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ni kuruhusu vyombo vya nje kufanya uchunguzi.
Lema ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 16, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Chadema Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Amesema haitakuwa aibu kwa Serikali kuhusisha vyombo vya nje kwa kuwa hata mataifa yaliyoendelea huwa yanaomba msaada inapobidi.
"Kama Serikali inaweza kuomba msaada wa Chandarua kwa ajili ya Malaria kwanini tunashindwa kuomba wasaidizi wa wa nje waje kutusaidia kuchunguza haya matukio ya kiharifu ili wananchi wawe na imani na Serikali .
"Kama serikali inataka kujiondoa katika lawama hizi za kutekwa kwa Mohamed Dewji basi tunaitaka iruhusu wachunguzi wa kimataifa kuja kufanya kazi ya kumtafuta Mohamed Dewji."Amesema Lema
Amesema kwa mazingira ya eneo ambalo Mo Dewji ametekwa kuna ulinzi wa hali ya juu, kushangazwa na mfanyabiashara huyo kutopatikana hadi sasa.
Lema pia amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kutozuia watu kujadili tukio hilo.
"Baada ya tukio la kutekwa kwa Mo Dewji Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe Kangi Lugola akatoka hadharani na kuwazuia watu kuongea habari za MO, kuzuia watu kuongea habari za kutekwa na kupotea ni kuzuia watu kulia wakiwa msibani, huu ni msiba.
"Kwa wajibu nilionao Mimi yale maneno ya Kangi kwamba wanasiasa tusitafute umaarufu kwenye tukio la MO Dewji ni ya kupuuza, niko tayari wanikamate lakini siwezi kukaa kimya.
"Hata kama nisingekuwa waziri kivuli nisingeogopa kuongelea swala la MO Dewji kwa sababu ya vitisho, ni bora kupiga kelele ili watu wengine wapone, siwezi kumuogopa Waziri wakati napigania maisha ya wanadamu wenzangu."Amesisitiza Lema
Jana, familia ya Dewji ilitangaza dau la Sh1bilioni kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.
Dewji alitekwa na watu wasiojulikana Alhamisi Oktoba 11, 2018 saa 11:30 alfajiri wakati akiwa Hoteli ya Colosseum.
Social Plugin